Imeandaliwa na; Aisha Bakari - TangaTV
Jumla ya Wazee 2703 wa Jiji la Tanga wamepatiwa kadi za bima ya afya ya jamii (CHF) leo. Zoezi la kugawa kadi hizo ambazo zimegusa kaya 1604, limefanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Tanga Jiji, liliongozwa na Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Akiongea kwenye zoezi hilo, Mhe Ummy aliwasifia Jiji la Tanga kwa kuwapa vitambulisho na kuwalipia wazee bima ya afya. “Tanga, nyie mmejiongeza, maana hamkuwapa wazee vitambulisho tuu, bali na kuwalipia kabisa bima ya afya ili kuweza kupata huduma za afya bila ya malipo, Kaimu Meya na Kaimu Mkurugenzi hongereni sana na kwa hakika Tanga hamjaniangusha.” Alisema kwa kusifia na kutoa pongezi.
Akiongeza juu ya kuwalipia wazee kadi ya bima ya afya, Mhe Ummy alisema ya kwamba Jiji la Tanga linaunga na Halmashauri ya Mji wa Kahama kuwa halmashauri pekee zinazowalipia wazee huduma ya afya, hakika wametekeleza maelekezo ya serikali kwa ukamifu. “Kwa kuwa na kadi ya bima ya afya kunamfanya mzee huyu kupata huduma zote za afya bure na bila ya kuwa na ule usumbufu wa kwenda kwa Mtandaji wa Kata na Mtendaji wa Mtaa ili aandikiwe barua”
Wakiongea na mwandishi wa habari hii, baadhi ya wazee waliopata kadi ya bima ya afya, waliishukuru Serikali kwa kuwaangalia kwa jicho la huruma na hakika wanaona Serikali yao bado inawajali na kuwathamini. “Mjukuu wangu, kwa umri wetu huu magonjwa ndio nyumbani kwake, sasa kama huna pesa na huna namna ya kupata matibabu hapo inakuwa mtihani. Japo suala la kufa ni ahadi ya Mwenyezi Mungu lakini kukosa matibabu kunachangia vifo vya haraka kwetu sisi wazee” alisema mmoja ya wazee hao.
Kuwapatia wazee huduma za afya bure ni agizo lilitolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kupitia agizo hilo Halmashauri zinatakiwa kuwapa wazee vitambulisho vya matibabu bure wazee wote wasio na uwezo ili kuwaondoshea usumbufu wanapokwenda hospitali kutibiwa.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.