Shirika lisilo la kiserikali la Legal and Advocacy Centre Initiative (LACI), lililosajiliwa mkoani Morogoro, na ambalo hufanya shughuli zake kitaifa, Ijumaa Julai 18, 2025, limetambulisha kwa Menejimenti ya Jiji la Tanga, mradi wa "Mtoto wa Mwenzako ni Wako, mlinde" utakao tekelezwa katika kata 27 za Jiji la Tanga, kwa kipindi cha kati ya miezi 12 hadi 24 kwa lengo la kuzuia aina zote za ukatili dhidi ya mtoto.
Akizungumzia shughuli zitakazo tekelezwa na mradi huo, Mkurugenzi wa LACI, Bi. Mourine Msangi, amesema mradi umejikita katika kufanya ulinzi wa mtoto kisheria, kuzuia vyanzo vya ukatili kwa kutoa elimu, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia manusura wa ukatili.
Msangi amewaomba wakazi wa Jiji la Tanga kuipa ushirikiano LACI itakapofika katika mitaa yao, ambapo amesema kwa nguvu ya pamoja ya jamii, upo uwezekano wa kuwalinda watoto dhidi ya aina zote za ukatili.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, katika tukio hilo, Bw. Simon Mdende, ameipongeza LACI kwa kuja na mradi huo, ambapo amesema Jiji la Tanga linatajwa kama moja ya miji yenye kiwango cha juu cha vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo shirika hilo litasaidia kupunguza hali hiyo, ambapo pia amewataka kuzingatia sheria na kanuni za usajili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.