Julai 8, 2025.
Morogoro.
Maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi maarufu kama nane nane, yanayofanyika kuanzia Augosti 01 - 08, kila mwaka, kwa mwaka huu wa 2025, yanafanyika ikiwa pia nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Uchaguzi mkuu, kwa mujibu wa katiba yetu, hufanyika kila baada ya miaka mitano. Na wakati wa uchaguzi mkuu, vyama hutoa "Ilani zao za uchaguzi" ambazo ni ahadi au mipango ya chama kwa wananchi iwapo kitashika dola, na chama chenye ilani nzuri, wananchi hukichagua kuongoza nchi.
Maonesho ya nane nane, hufanyika kwa kanda. Moja ya kanda hizo, ni kanda ya Mashariki, inayojumuisha Mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga, na hufanyika katika Uwanja wa maonesho wa Mwl. J. K. Nyerere, uliopo Manispaa ya Morogoro. Maonesho hayo kwa mwaka huu, 2025, yanabeba kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025"
Halmashauri ya Jiji la Tanga ni moja ya Halmashauri zinazounda kanda hiyo, na mwaka huu, imejipanga kushiriki maonesho hayo kwa kuonyesha kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuleta mapinduzi kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi.
Halmashauri ya Jiji la Tanga imefanikiwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama tawala (Chama cha Mapinduzi) katika maeneo tofauti, ikiwa ni pamoja na hili la kilimo, mifugo na uvuvi. Mafanikio haya ambayo yatawasilishwa kwa takwimu katika nane nane mwaka huu, kwenye banda la maonesho la Jiji la Tanga, yataonyesha hali ilivyokuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, na mafanikio yaliyofikiwa sasa, na kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kujenga uchumi wao na ustawi wa taifa.
Katika banda hilo, wananchi wataweza kuona namna Halmashauri ilivyotekeleza lengo la kukifanya kilimo kinakuwa cha kisasa na cha kibiashara, ili kuhakikisha kuwa Taifa linajitosheleza kwa chakula, kuimarisha uchumi, kuongeza kipato cha wakulima, kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda na kuongeza ajira.
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini, amewaalika watu wote watakao weza kufika katika uwanja wa maonesho wa Mwl. J. K. Nyerere, Manispaa ya Morogoro, kufika katika banda la Jiji la Tanga kuweza kujionea mapinduzi hayo makubwa ya kilimo, ufugaji na uchumi wa bluu yatakayowasilishwa na wataalamu wa Halmashauri hiyo.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.