Julai 21, 2025.
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini, amekabidhi magari mapya manne yenye thamani ya shillingi million 661 yaliyonunuliwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga katika bajeti ya mwaka 2024/2025, kwa wakuu wa idara na vitengo, kwa ajili ya kusaidia utendaji kazi wa sehemu hizo.
Magari hayo yamekabidhiwa kwa idara ya Utawala magari mawili (coaster na double cabin pick up), Idara ya Mipango na Uratibu, gari moja (double cabin pick up) na vitengo viwili vya Ukaguzi wa Ndani na cha Manunuzi, wakikabidhiwa gari moja, ( double cabin pick up) kutokana na shughuli zao za ufuatiliaji wa miradi, kufanyika kwa pamoja.
Akizungumza baada ya kukabidhi gari hizo, Mhandisi Hamsini amelishukuru baraza la madiwani lililomaliza muda wake kwa kuridhia ununuzi huo kwa kupitisha bajeti.
"Kwa leo tumekabidhi gari 4 zenye thamani ya milioni mia sita sitini na moja, hii inaleta tija kwa watumishi katika kusimamia miradi ya maendeleo na kupata safari za kikazi, kumbuka kazi nyingi tunazokwenda ni Dar es salaam pamoja na Dodoma, ni aibu kubwa sana kwa mtumishi ambaye ni senior (mwandamizi) kupanda basi, kwahiyo tukasema haiwezekani. Lazima kipaumbele chetu tuhakikishe tunakuwa na magari kwa ajili ya shughuli zetu......
.......Lakini vitendea kazi hivi vilivyotolewa sio kwa ajili ya kuchezea ni kwa ajili ya kusimamia kazi za Halmashauri kwa niaba ya wananchi wa jiji la Tanga, lakini kununua gari ni hatua moja wapo, kuitunza gari ni kitu muhimu sana gari ni kama binadamu inahitaji chakula, chakula chake ni oil na spare parts, unatakiwa uweke spare parts na oil ambazo ni original sio unanunua vitu mtaani kwahiyo lazima zipelekwe kwenye gereji ambazo zimeainishwa na mzabuni husika.
Kwahiyo nawasisitiza wenzangu leo magari yapo lakini tuhakikishe tuyatunze japo yatumike miaka mitatu mpaka mitano" Amesisitiza Mhandisi Juma Hamsini.
Katika bajeti ya mwaka huu 2025/2026, Halmashauri inakusudia kununua gari mpya tatu na mitambo, ikiwemo gari maalumu ya matangazo kwa ajili ya kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.