Mradi wa uboreshaji mazingira ya utoaji elimu nchini(SHULE BORA) unaotekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Misaada la Uingereza (UKaid), umeendesha mafunzo kwa Walimu Wakuu, Wenyeviti wa Kamati za Shule, pamoja na Maafisa Elimu Kata wa Jiji la Tanga kwa lengo la kuwapatia uelewa, mbinu na miongozo ya uanzishaji, utekelezaji na usimamizi wa Ushirikiano wa Wazazi na Walimu (UWAWA) katika elimu ya awali na msingi.
Akifungua mafunzo hayo ya siku tatu, yaliyoanza leo, Jumatatu Machi 13, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri, Afisa Elimu Awali na Msingi wa Jiji la Tanga, Mwl. Kassim Kaoneka amesema lengo la kuunda umoja huo ni kuwaleta pamoja walimu na wazazi katika kusaidiana ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya kujifunzia na kufunzia.
"Kufanya vizuri kwa mtoto au kufanya vizuri kitaaluma, kunamtegemea mwanafunzi mwenyewe, Mwalimu, Mzazi au Mlezi, lakini na mazingira yote, hata njia anayoitumia kwenda na kutoka shule. Vyote hivyo vinachangia katika kufanya vizuri kwenye taaluma au kufaulu kwa mtoto" Amesema Kaoneka.
Kaoneka amesema umoja huo wa ushirikiano wa wazazi na walimu utasaidia kuimarisha usimamizi na uendeshaji katika utoaji wa elimu ya awali na msingi kwa kupunguza utoro, mdondoko wa wanafunzi na kuimarisha elimu jumuishi.
"Mtoto anatakiwa awahi shule asubuhi, akichelewa atavikosa vipindi vya mapema, mtoto anatakiwa apate sare za shule, mtoto anatakiwa asiwe mtoro, na ili asiwe mtoro, Mazingira shuleni yanatakiwa kuwa mazuri, ili asiwe mtoro, shuleni kuwe na chakula". Ameeleza Kaoneka.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, wameeleza matumaini yao kwa kuanzishwa kwa uWAWA kwamba utaleta ushirikiano mzuri kati ya wazazi na walimu na hivyo kuboresha utendaji na kuinua kiwango cha taaluma.
Mradi wa SHULE BORA ni program mpya ya elimu inayolenga kuinua ubora wa elimu jumuishi inayotolewa kwenye Mazingira salama ya kujifunzia kwa wasichana na wavulana kwenye shule za umma nchini chini ya shirika la Misaada la Uingereza (UKAID) na kutekelezwa katika mikoa tisa ya Tanzania Bara.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.