Waziri wa mifugo na uvuvi Luhaga Mpina amewataka wavuvi kuendelea kufuata kanuni na sheria za uvuvi zilizowekwa na Serikali ili kuendelea kupata samaki wakubwa katika Bahari ya hindi.
Akizungumza na wavuvi wa soko la deep sea Jijini Tanga Waziri Mpina aliwahimiza kutotumika vibaya na viongozi wanaokuja kuomba kura huku wakiwadanganya kuvunja sheria ya uvuvi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 28 mwezi wa kumi mwaka huu.
“Niwashukuru sana wananchi kwa jitihada mnazozifanya za kuhakikisha mnavua kwa nyavu halali tuendelee kuunga mkono jitihada za Serikali ili uvuvi wetu uendelee kutupa manufaa na kwa wale ambao wanasema kipindi hiki ni cha uchaguzi kwahiyo hawatakamatwa niwambie tu kuwa sheria bado ipo vilevile hata kama tunaelekea katika uchaguzi ”Alisema Waziri wa mifugo na uvuvi Luhaga Mpina
Sambamba na hayo pia Waziri Mpina alitoa onyo kwa wagombea wa Jiji la Tanga kutowatumia vibaya wavuvi wa Jiji hili kwani Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli haina lengo la kuwaonea wananchi .
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji alieleza ni kwa namna gani wamejipanga katika kuboresha miundombinu ya wavuvi kwa kutenga kiasi cha shillingi Milion 250 ikiwa ni kuboresha njia kwaajili ya mabasi yanayosafirisha mizigo ,kuboresha jengo linalotumia kuuza samaki .
“Mbali na hayo tuna mipango mipana katika kutaboresha barabara ili magari yanayokuja kuleta mizigo yaweze kuja bila wasiwasi pili tutaboresha jengo la kuuzia samaki kwasababu limekuwa bovu na tutatengeneza eneo la muda mfupi ili hili tulibomoe na kujenga upya “Alisema Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji
Mayeji aliongeza kwa kumwomba Waziri wa mifugo na uvuvi Luhaga Mpina kuwafikiria wavuvi wa Jiji la Tanga katika mpango wa kuanza mfumo wa uvuvi katika maji marefu kwa kuwa Tanga kuna Bahari pana na yenye maji marefu na samaki wengi wazuri .
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.