Mwenyekiti wa Kamati ya kudhibiti UKIMWI Jiji la Tanga, Mhe. Mwanaidi Kombo ameshauri kutengwa kwa muda ndani ya vipindi vya dini vinavyofundishwa katika Shule za Msingi na Sekondari, kwa ajili ya kutoa elimu ya masuala ya Ukimwi na kupiga vita aina zote za unyanyapaa.
Ushauri huo ameutoa leo, jumatatu Oktoba 17, 2022 wakati akifungua kikao cha ziara ya Kamati kutembelea shughuli zinazofanywa na wadau katika kupambana na Ukimwi ndani ya Jiji la Tanga.
Mheshimiwa Kombo, ambaye pia ni Naibu Meya wa Jiji la Tanga na Diwani wa Viti Maalum kutoka Kata ya Central, amesema kama viongozi wa dini wakitumia sehemu ya muda wao wawapo katika vipindi mashuleni kwa kutoa elimu ya kujikinga, athari na kuzuia unyanyapaa, itasaidia kuwajenga vijana na kujitambua mapema.
Kamati ya Kudhibiti Ukimwi ambayo inaundwa na baadhi ya Madiwani, Asasi zinazoshughulikia Ukimwi, wadau na baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo vya Halmashauri, imetembelea Kituo cha 4H Kange, Kamati ya Ukimwi Kata ya Usagara na kukutana na Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (KONGA), pamoja na Waraibu wa dawa za kulevya wanaoendelea kupata nafuu.
Katika Kituo cha 4H Kange, kamati ilijionea mradi wa kuwawezesha ujuzi wasichana waliopata ujauzito shuleni na kukatiza masomo yao, ambapo kituo kinawafundisha kazi za ushonaji nguo na elimu ya afya, wahitimu wakizawadiwa cherehani.
Akizungumzia utendaji wa Kamati za Ukimwi ngazi ya Kata, Mratibu wa Ukimwi kwa Jiji la Tanga Bw. Moses Kisibo amezitaka Kamati hizo kufanya kazi kwa bidii kuisaidia jamii na kwamba wawatake madaktari kuwapa takwimu za hali ya maambukizi mapya katika maeneo yao ili kuwa na taarifa iliyokamili.
Kamati ya Ukimwi kupitia Jiji la Tanga inakusudia kutoa ruzuku kwa vikundi vya KONGA na Waraibu wa dawa za kulevya ili kuwawezesha kuanzisha miradi ya kiuchumi.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.