Pamoja na kusimamia miradi mingine ya maendeleo, Halmashauri ya Jiji la Tanga inazingatia kutenga asilimia 10 ya makusanyo halisi ya mapato ya ndani kwaajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake kwa asilimia 4%, vijana 4%, na watu wenye ulemavu 2%, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 jiji la Tanga imetoa mikopo yenye thamani ya Tshs.850,343,274 ambayo ni sawa na asilimia 100 ya makusanyo halisi, fedha hizo zimekopeshwa kwa Vikundi 73 vya wanawake, vikundi 25 vya vijana na watu wenye ulemavu vikundi 6, na tutaendelea kuwezesha vikundi hivi kwa kadri iwezekanavyo. Alieleza Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji alipokuwa akifanya mahojiano na Afisa Habari.
Kikundi cha Winners Women Group ni miongoni mwa vikundi 73 vilivyonufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri ambacho kimetokea kata ya Mzingani kimesajliwa 2017 kwa idadi ya wanakikundi 30 wote wakiwa wanawake, kwa mtaji wa Tshs.47,000,000/= ambalo ni ongezeko la mtaji baada ya kukopeshwa Tshs.Mil.20 ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ujasiriamali kama ufugaji nyuki, ufugaji wa kuku, kutengeneza batiki, sabuni za maji na kikoba huku kiasi cha Tshs.10,334,000/= kimeifadhiwa benki.
“Kutokana na Mtaji kuongezeka tumeweza kurejesha Tshs.16,000,000/= kati ya Tshs.20,000,000/= tulizokopa na hivyo kubakia na deni la Mil.4 tu, aiseee tunaishukuru sana Serikali kwa kutuunga mkono wanawake pale tunapoonyesha juhudi kwani kwakweli tunasomesha watoto, tumeboresha biashara zetu za mtu mmoja mmoja kwasababu tumeongeza mitaji yetu.” Alisema Mwenyekiti wa Kikundi hicho Bi. Fatuma Sheshe
Naye Mweka Hazina wa kikundi hiko Bi. Mary Mshote ameishukuru sana Halmashauri ya jiji la Tanga na kumshukuru zaidi Rais Mhe.John Pombe Magufuli kwa kuwa yeye binafsi kupitia mikopo wanayopata na kufanya shughuli ambazo zimewaingizia kipato ameweza kumsomesha kijana wake chuo kikuu lakini pia amebainisha changamoto ya ufinyu wa muda wa marejesho hali ambayo usababisha wakimbizane kuhakikisha wanarejesha kwa wakati.
“Nilikuwa nasikiaga tu habari za mikopo kwa wanawake kutoka Halmashauri hata sikuamini mpaka pale nilipojiunga na kikundi chetu na tukapata mkopo ambao kwakweli umetusaidia pakubwa mno sisi wakina mama, ila tunaomba Serikali ituongezee muda wa marejesho kwani muda tunaopewa sasa ni mdogo, sisi tumekopa Mil.20 ila tunarejesha ndani ya mwaka mmoja, naamini itatufikiria ili wamama tuendelee kupambana na kutumia mikopo hiyo kwa tija,”. Alisisitiza Bi. Mshote
Vifaranga vya kuku katika Banda la Kikundi cha Winners Women Group.
Mweka Hazina wa Winners Women Group akilisha kuku wanaowafunga kama moja ya shughuli zao katika Banda lao.
Winners Women Group wakitengeneza Sabuni.
Sabuni iliyotengenezwa na Winners Women Group ikiwa inachanganywa.
TUINI Women Group pia ni kikundi cha wanawake kinachopatikana kata ya Maweni ambacho kimesajiliwa 2010, chenye idadi ya wanavikundi 30huku shughuli zao zikiwa ni utengenezaji wa Batiki , Jiki, Sabuni za maji na Vicoba lakini lenye kuvutia zaidi katika TUINI women group ni kuajiri vijana 12 baada ya kununua pikipiki 12 na kununua shamba la Heka 15 lilipo Maramba wilayani Mkinga, kikundi hiki kutokana na kuwa na urejeshaji mzuri na matumizi yenye tija kimepata mkopo kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza walikopeshwa Tshs.15,000,000/= na awamu ya pili waliongezewa Tshs. 25,000,000/= ili kuendelea kuimarisha shughuli za kikundi hiko.
“ Sisi TUINI Women Group kwakweli ni wanufaikaji wakubwa sana wa Serikali ya awamu ya tano kwani kuanzia 2018 tumepata mkopo Tshs.15,000,000/= ikiwa ni awamu yetu ya kwanza hatukutaka kuangusha serikali kabisa ule mkopo tuliufanyia kazi kama tulivyodhamiria kuomba ndipo 2020 tukaongezewa tena Tshs.25,000,000/= baada ya ofisi ya maendeleo ya jamii ya jiji kuona tupo siriazi kujiongezea kipato, sasa tuna shamba heka 15 Maramba Mkinga, tumenunua pikipiki 12, tumeongeza vifaa vya Uzalishaji wa kutengeneza Batiki kwani tunaandaa sare za siku ya wanawake duniani, kanisani na kwenye makongamano, na kipato binafsi cha kila mwanakikundi kimeongezeka sana sana na tunasomesha watoto 5 wasiokuwa na uwezo,”. Alisema hayo Mwenyekiti Bi. Edita Nauli alipotembelewa na Afisa Habari wa Jiji la Tanga
Bi. Zera William akiipua batiki baada ya kupikwa jikoni.
Bi. Zera William akizipika Batiki zinazotengenezwa na kikundi hiko.
Batiki ikiwa inaanza kuchanganya rangi kabla ya kupelekwa kuanza kupikwa.
Batiki ya kikundi cha TUINI ikiwa imetoka kuchanganywa.
Batiki ikiwa tayari imetengenezwa tayari kuanikwa na kwenda kuuza.
TUINI Women Group kwenye picha ya pamoja na baadhi ya vijana wa bodaboda waliowaajiri.
Aidha Mwenyekiti amebainisha changamoto kubwa wanayokutana nayo ni masoko ya batiki hizo kwani batiki wanazotengeneza zina viwango vya juu lakini soko limekuwa sio la kuridhisha sana tofauti na matarajio yao japo hawajakata tamaa, kwani kutokana pia na ugumu wa upatikanaji wa malighafi za utengenezaji wa batiki lakini bado wanaendelea kutengeneza.
“Bado watanzania hawajahamasika kushona sare za batiki kama wanavyoshona vitenge hali hii hupelekea soko la batiki kuwa sio la uhakika, ilanatamani watu wajue kuwa batiki ni nzuri na ni za kipekee sana unaweza ukachanganya rangi unazotaka wewe na ukawa peke yako na hivyo kupandisha soko la batiki,”. Alisisitiza Mwenyeikiti huyo
Naye Mwanakikundi Bi. Zera William amesema anatamani sana kutembelewa na Mhe.John Pombe Magufuli ili kutoa shukrani zake za dhati kwani binafsi amenufaika sana na mikopo wanayopewa na Halmashauri “Nasomesha wanangu, chakula sio shida tena kwetu nina uhakika wa milo mitatu hii yote ni kwaajili ya mikopo hakika ninamuombea uzima Mhe. Rais na Mkurugenzi wa jiji la Tanga,”. Alisema Bi Zera.
Vijana ambao ndio tegemeo la Taifa nao hawakuachwa nyuma katika mikopo hii ili waweze kujenga Taifa lenye Uchumi wa kati lakini lenye nguvu na ubunifu mkubwa, tuelekee kwa Vijana wa pale Mwakidila.
Mwakidila Chapakazi Youth Group ni kikundi cha Vijana kilichoanzishwa 2015 kilichopo kata ya Tangasisi mtaa wa Mwakidila B, kikiwa na wanachama 11 wa kike wakijishughulisha na ufyatuaji wa matofali na kilimo cha matunda hususani Tikiti. Mwakidila Chapakazi walikuwa na mtaji wa Tshs.5,200,000/= wakakopeshwa na Halmashauri Tshs.10,000,000/= ambazo wameziendeleza kwenye kilimo kwa kununua shamba la heka moja lililopo Chongoleani, pamoja na kuajiri vijana wenzao wengine 10 katika ufyatuaji wa matofali, Katibu wa kikundi hiki wakati akizungumza na Afisa Habari amesema mkopo walioupata umeleta mafaniko makubwa sana kwao, kwani sasa wanakikundi wana viwanja ambavyo kila mmoja amenunua kama faida yake binafsi lakini pia wanasomesha watoto na wadogo zao Sekondari.
“ Kuna msemo unasema vijana ni tegemeo la kesho la Taifa, Sisi Mwakidila tunasema ni tegemeo la sasa na kwakuona hilo ndiyo maana Serikali ya Magufuli ilivyoingia madarakani 2015 tukaanzisha kikundi chetu ambacho pia kina mwanamke mmoja, “jembe letu” ili tupate mkopo na tumepata kama unavyoona tunafytua matofali, tumeajiri vijana wenzetu 10 watusaidie, lakini tumenunua shamba heka 1 Chongoleani, kwa shughuli zetu hizi tumeweza kununua viwanja na kusomesha wanetu na wadogo zetu sekondari, binafsi nikisikiaga wimbo wa Magufuli jembe uwa nafurahi sana sababu ujembe tumeuona kupitia Halmashauri yetu ya jiji maana wengi wetu tumetoka chuo tukaona tujiajiri na Maisha yanasonga,”. Alisema Mwenyekiti Bw. Nasibu Musa
Mimosa wa vijana walioajiriwa na Mwakidila Chapakzi Youth Group akiwa amebeba tofali.
Mwenyekiti wa Kikundi Ndugu Nasibu Musa akiwa anapanga Matofali.
Mmoja wa Wateja waliofika kununua Tofali hizo ambaye jina lake halikufahamika.
Mifuko ya Simeni ya Wanakikundi ikiendelea na kazi ya kufyatua Matofali.
Baadhi ya Wanakikundi cha Mwakidila Chapakazi Youth Group na vijana wenzao walioajiri.
TAYOTAI ni kikundi cha vijana wa kike kinachojishughulisha na ushonaji wa nguo za aina mbalimbali, ambacho kinapatikana kata ya Makorora eneo la Community Center kama Tanga Youth Tailoring (TAYOTAI), ambacho kimenufaika na mkopo unaotolewa kwa vijana, kimesajiliwa 2019 kikiwa na jumla ya wanakikundi 32, kikundi hiki kimepata mkopo wa Tshs.100,000,000/= ambao ulitumika kununua Vyerehani za kisasa vinavyotumia umeme na kuanzisha mtaji wa shughuli za Ushonaji kama Sare za Shule, Manesi, pia kushona nguo za mitindo mbalimbali yenye ubunifu.
“ Tunapenda kuendelea kuishukuru serikali kwa mkopo waliotupatia sisi vijana wa kike ambao wengi wetu tuna umri kuanzia miaka 19 mpaka 35, tulikuwa tunakaa tu nyumbani bila shughuli yoyote ile hali iliyokuwa inatupelekea kuwa wake za watu katika umri mdogo na kuwa tegemezi kwa wazazi, lakini sasa tuna ofisi ambayo tumepewa na jiji, pia tuna ujuzi wa kushona kwa mashine ya kudarizi ambao tumeongezewa na Serikali kupitia Halmashauri ya jiji la Tanga, kiasi tumekuwa tukipata tenda katika baadhi ya shule na vituo vya Afya kama Galanos sekondari, kituo cha Afya Duga, Mikanjuni, Makorora, na Masiwani,” Alisema Fatma Amiri Katibu wa kikundi hiki
Maimuna Said Binti akiendelea kushona nguo ya mteja .
Mwanakikundi akiendelea na ushonaji kwa cherehani inayotumia Umeme.
Mwanakikundi Mariam Seleman akiendelea na ushonaj wa Sare za Shule.
Wanakikundi wakiwa katika shughuli zao za kila siku za Ushonaji katika ofisi yao Makorora Community Centre.
Akizungumza na Afisa Habari wa jiji Mwenyekiti wa TAYOTAI Bi.Lilian Michael amesema japokuwa kikundi kina ujuzi na cherehani za kisasa kimekuwa na changamoto ya kupata tenda za mara kwa mara pamoja na kuwa wanaendelea kujitangaza kupitia redio zilizopo jiji la Tanga na kituo cha Tanga Televisheni na katika ukurasa wao instagram,”Mafanikio kiukweli ni mengi na makubwa, kwanza kitendo cha kuamka tu na kujua unaelekea ofisini, pili tumepata ujuzi mwingi juu ya masuala ya rasilimali watu na fedha, elimu ya kujitambua, ujuzi wa kutumia cherehani ya umeme, mashine ya kudarizi na kupata tenda ni vitu ambavyo kiukweli mimi binafsi sikuwahi kuwaza kabisa , tunamshukuru Mkurugenzi kwa fursa hii, lakini tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. John Magufuli najua wengi tulionufaika lazima tushukuru sababu faida zake tunaziona, “. Alisisitiza Mwenyekiti
Mwenyekiti wa Kikundi cha TAYOTAI Bi. Lilian Michael akiwa katika ushonaji.
Tanga One Youth ni miongoni pia mwa vikundi vya vijana vilivyonufaika na mikopo inayotolewa, kikundi hiki kilipata mkopo wa Tshs.182,000,000/=, mkopo ambao umetolewa kwa vijana 70 katika kikundi kilichosajiliwa 2019, kinachojishughulisha na usafirishaji wa abiria maarufu kama “Bodaboda” ambapo fedha ya mkopo ilitumika kununua pikipiki 70 pamoja kulipia bima, kununua mafuta ya kuanzia na vibali vyote vinavyohusika.
“Kwa hili Mhe.Rais Dkt.John Magufuli na Halmashauri ya Jiji la Tanga wametukomboa sana vijana wa Tanga kwani sasa tuna uhakika wa kipato cha kila siku, tunaendesha maisha yetu kwa kazi yetu ya boda boda, maana hizi tukimaliza kurejesha zinakuwa ni zetu kabisa, na tunauhakika wa kumiliki pikipiki zetu wenyewe kwa gharama nafuu na kuacha kutegemea pikipik ya mtu ambaye anakupa pikipiki yake kwa masharti magumu kwa siku 10,000/= wakati huku huku jiji tunarejesha kwa 6500/= tu tena bila riba,ama kwa hakika Serikali ya awamu ya tano inatuthamini sana vijana, sisi Tanga One Youth ni mashahidi ,”. Alisema Omary Ahmed Kusaka katibu wa Kikundi hiki
Picha ya baadhi ya Wanakikundi cha Tanga One Youth walionufaika na Mkopo ambao walinunua pikipiki.
Katika vikundi vingi vya vijana wadau wanasema kuna changamoto kwa kuwa kila kijana uwa na mtazamo wake, tungependa kufahamu changamoto gani kama vijana wa Tanga One Youth mnapitia? Alihoji Afisa Habari wa Jiji.
“Changamoto kwenye vikundi vya vijana hazikosekani, ila tunajitahidi mara kwa mara kukumbushana nia njema ya Serikali kwa vijana hususani kwa sisi vijana wa Tanga ambao tumepata neema hii, kuna wengine uwa wanasumbua kurejesha mpaka watafutwe sana lakini mwisho wa siku wanarudi kwenye mstari na kurejesha, maana tukirejesha kwa wakati tutaendelea kuaminika na kukopeshwa awamu nyingine ya pili,”. Alisema Katibu
Katika mgawanjo wa asilimia 10, Serikali iliweka 2% kwaajili ya watu wenye ulemavu ambao nao wanajiunga katika vikundi na kuanzisha shughuli ambayo kwa pamoja watachukua mkopo nan a kuendeleza shughuli hiyo.
Tanga Viziwi Group ni kikundi kimojawapo cha watu wenye ulemavu kati 6 ambacho kinapatikana Makorora, kimesajiliwa mwaka 2018 kikiwa na wanachama 8, kikijishughulisha na utengenezaji wa Samani, kupiga picha za mnato na ufundi wa umeme, kuchomelea mageti.
Kilipotembelewa kikundi hicho eneo la dunia hotel, Katibu wa kikundi Ndugu Hussein Juma amesema licha ya changamoto mbalimbali walizokutana nazo lakini wameweza kuzikabili na kufanikiwa kurudisha Tshs.10,000,000 ikiwa ni mkopo ambao hauna riba, kwao ni fanikio kubwa sana, kwani hata sasa wanajipanga kufanya mchakato wa kuomba mkopo tena ili kuendelea kuboresha kikundi chao zaidi ambacho kila mwanachama amenufaika binafsi kwa kuwa na uhakika wa kipato cha kila siku na familia zao, pia kusomesha watoto.
“Kila mwanachama anafurahia mkopo huu kwani umeweza kuturahisishia shughuli zetu sana kwakuwa mkopo huu wa Serikali hauna riba tofauti na mikopo mingine ambayo ina masharti makali kwa sisi inakuwa inaumiza, leo hamjatukuta wote sababu ya majukumu na dharura walizopata wenzangu ila ungesikia ni namna gani tumewezeshwa na tutaendelea kuwezeshwa kwa mikopo hii ambayo sisi tushamaliza hadi kulipa Mil.10 tuliyokopeshwa,”. Alisema Katibu
Ndugu Hussein Juma ambaye ni Katibu wa Kikundi cha Tanga Viziwi Group akisafisha picha za mteja.
Aidha Ndugu Hussein Juma amemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano kwa kufanya kazi kwa juhudi na kuendelea kutetea maslahi ya watu wa chini hususani wa makundi maalum.
Upande wake Afisa Maendeleo wa Jiji Ndugu. Simon Mdende amesema kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imeendelea kusajili vikundi, kutoa elimu kabla ya kutoa mkopo na baada ya kutoa ili kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa ili wengine wakope, pia kutatua changamoto zilizopo ndani ya uwezo waona nyingine kuwasilisha zinapohusika wao wakiwa waratibu wakuu, aidha kutoa mafunzo ya ujasiriamali kupitia makongamano mbalimbali, na kuviwezesha vikundi hivyo kiuchumi kwa kuvitafutia masoko ndani na nje ya Tanga,lakini pia kuhakikisha vikundi vinashiriki maonesho mbalimbali.
“Idara ya Maendeleo ya Jamii inalenga kuikomboa jamii kata nyanja zote, leo tukiongelea vikundi uwa tunahakikisha vikundi vinashiriki maonesho mbalimbali ili kutangaza bidhaa zao, mwaka jana 2020 TAYOTAI ilishiriki maonesho ya 88, pia vikundi viwili vipo mkoani Arusha sasa kwenye Maonesho ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, vilevile tumesaidia vikundi kupata masoko mfano kuna kikundi cha Uvuvi kilichopo Makorora sasa kinapeleka samaki Mafinga Iringa,”. Alisema Mdende
Hata hivyo kumekuwa na ucheleweshaji wa marejesho kwa baadhi ya vikundi huku wengi wakisema ni kutokana a muda mchache waliopewa kurejesha fedha hizo, Afisa Maendeleo amesema hali hiyo ya ucheleweshaji uwalazimu kutotoa tena mikopo kwa awamu ya pili kwa vile vikundi ambavyo vinasumbua sana kurudisha mikopo ambayo serikali utoa bila riba ili wengine wakope.
“Muda wa kurejesha upo katika Sheria, uwa tunawaelimisha kuwa muda upo kisheria ni mapaka ibadilishwe vinginenvyo inawapasa kuendelea kufuata sharia ya kurudisha mkopo ndani yam waka mmoja japokuwa kwa kikundi kama cha TAYOTAI, na TANGA ONE YOUTH ambacho vimekopeshwa zaidi ya Mi.100 vimeongezewa muda wa marejesho, lakini pia tunaendelea kutoa ushauri kwa mamlaka za juu yetu zenye dhamana kuendelea kufikria kuhusu kuongea muda wa marejesho,” Alifafanua Afisa Maendeleo.
Pia Afisa huyo amesema kuna changamoto ya ugumu wa kuunda vikundi vya kiuchumi vya watu wenye ulemavu kwani jamii bado inawaficha na ukizingatia kanuni ya mikopo inataka vikundi vwe na watu kuanzia 10 hali inayopelekea kupata watu hao kwa idadi hiyo wanaoaminiana, Afisa maendeleo ameshauri ni vyema idadi ya kikundi kwa kundi hili maalum zaidi kuwa watu 5.
Halmashauri ya jiji la Tanga kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imetenga kiasi cha Tshs. 1,225,305,864/= kwaajili ya kutoa mikopo kwa vikundi. Katika robo ya kwanza Julai-Septemba, Halmashauri imetoa mikopo yenye jumla ya Tshs.228,500,000/=, huku vikundi 29 vya wanawake kiasi cha Tshs.167,000,000/=, vikundi 7 vya Vijana Tshs. 48,000,000 na Vikundi 2 vya watu wenye ulemavu Tshs.13,500,000/=, huku ikiendelea na mchakato wa kukamilisha utoaji wa mikopo kwa robo ya pili Oktoba-Desemba 2020/2021 kiasi cha Tshs. 300,000,000/= ambayo itatolewa mwishoni mwa mwezi Januari 2021.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.