Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Bw. Said Majaliwa amezitembelea timu za mpira wa miguu na netiboli (pete) za Jiji la Tanga zinazojiandaa na mashindano ya michezo na sanaa za maonesho, ya Shirikisho la Michezo ya Watumishi wa Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA), yanayotarajiwa kufanyika baadae mwezi huu, huko Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Majaliwa alianza kwa kuitembelea timu ya netiboli (netball) inayofanyia mazoezi yake katika Uwanja wa Polisi Chumbageni, baadae alielekea Uwanja wa Shule ya Sekondari Galanos, sehemu inapofanyia mazoezi timu ya mpira wa miguu.
Akiwa katika viwanja vyote hivyo, Majaliwa alipata nafasi ya kuangalia mazoezi ya timu hizo, na baadae kuongea na wanamichezo hao, ambapo alieleza kuridhishwa kwake na maandalizi yanayoendelea, na aliwaahidi kuwa pamoja nao katika kipindi hiki cha maandalizi na wakati wote wa mashindano, huku akiwataka kuzingatia mazoezi na kuwaheshimu walimu wao (makocha), ili timu hizo zirudi na ushindi.
Mkurugenzi Majaliwa ambaye ni mwanamichezo na ambaye pia aliwahi kuwa kiongozi katika michezo, amewataka wanamichezo hao kuliwakilisha Jiji vizuri kwa kuwa na nidhamu wakati wote wa mashindano. Amesema hatafurahi kusikia mtumishi kutoka Jiji la Tanga akionekana au kupatikana katika matendo yasiyofaa kwa mtumishi wa umma, hivyo wanapaswa kuzingatia nidhamu wakijua wanaiwakilisha Halmashauri yao.
Mkurugenzi Majaliwa ametoa ahadi ya kuinunulia timu ya mpira wa miguu viatu vipya vya kuchezea mechi ya kwanza, kama chachu ya kuamsha ari ya wachezaji hao.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga aliongozana na Afisa Michezo wa Jiji, Bw. Michael Njaule, Kiongozi wa Timu, Bw. Jamal Minja, Afisa Utumishi Bw. Ally Ulaya na Afisa Habari wa Jiji, Bw. Mussa Labani.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.