Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (INEC), imefanya Mkutano na Wadau wa uchaguzi katika mkoa wa Tanga, kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, mkutano ulioongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jacobs Mwambegele, na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka vyama vya siasa, vyama vya wenye ulemavu, viongozi wa dini, mila, taasisi, Serikali na wadau wengine.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, uliofanyika Jumamosi ya Februari 01, 2025 katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mwambegele amewashukuru wadau wa uchaguzi waliohudhuria mkutano huo kwa namna ambavyo wamekuwa wakiipa Tume ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake, hata katika kipindi hiki cha uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Amesema uboreshaji utafanyika kwa siku saba, kuanzia Februari 13 hadi 19, 2025 na kituo cha kujiandikishia kitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Jaji Mwambegele amewaasa wananchi kujiepusha na kosa la jinai la kujiandikisha zaidi ya mara moja, kwani adhabu yake ni faini isiyopungua shillingi 100,000 na isiyozidi shillingi 300,000 au kifungo gerezani kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili, au vyote kwa pamoja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani, amesema zoezi hilo litahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na wale watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu 2025, na kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika.
Amesema zoezi litatoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine, na kutoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye Daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali.
Uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura pia utahusisha kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo
kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na kifo.
Kauli mbiu ya zoezi hilo inasema, "Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora".
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.