Januari 9, 2025.
Halmashauri ya Jiji la Tanga imeanza kutekeleza mpango wake wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa majengo ya ghorofa, ambapo kwa mwaka huu wa 2024/2025, shule nne za msingi za Mbuyuni, Majengo, Martin Shamba na Ngamiani Kusini, zimewekwa kwenye mpango wa ujenzi wa majengo hayo, na tayari kazi hiyo ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, leo alhamisi, Januari 9, 2025, ikiwa katika ziara yake ya kawaida ya kila robo mwaka ya kukagua shughuli zinazotekelezwa na Idara na Vitengo vya Halmashauri vinavyo simamiwa na Kamati hiyo, ilitembelea ujenzi wa jengo la madarasa ya ghorofa linalojengwa katika Shule ya Awali na Msingi ya Mbuyuni iliyopo kata ya Nguvumali, ambapo ilipokelewa na uongozi wa Mtaa, Shule na kamati za ujenzi.
Akizungumzia ujenzi huo, Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Dorothy Mapunda, amesema ujenzi wa jengo hilo ambalo tayari limeingiziwa shillingi million 350, litakapokamilika, litawapatia wanafunzi na walimu, mazingira mazuri ya kujifunzia na kufunzia, kwani majengo ya awali yalikuwa ni hatarishi kutokana na uchakavu wake.
Jengo hilo litakapo kamilika, litakuwa la ghorofa mbili(sakafu tatu) zenye vyumba 12 vya madarasa( vinne kila sakafu), vyoo na ofisi za walimu. Shule ya msingi Mbuyuni ina jumla ya wanafunzi 402.
Katika ziara hiyo, Kamati iliongozwa na Kaimu Mwenyekiti Mhe. Selebosi Mustafa, ilitembelea na kukagua eneo la ujenzi wa Zahanati ya Msambweni kata ya Msambweni, eneo la dampo Mwang'ombe, kata ya Tangasisi, ambalo Halmashauri inakusudia kupabadilisha matumizi kwa kujengwa viwanja vya michezo vya kisasa.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.