Na: Mussa Labani, Tanga.
Halmashauri ya Jiji la Tanga inakusudia kutumia kiasi cha zaidi ya shillingi million 18 kukarabati soko la Mgandini ili kuondoa changamoto za miundombinu ya njia, vyoo, ikiwa ni pamoja na maboresho ya vizimba vya nazi, ili kuwawezesha wafanyabiashara wa soko hilo pamoja na wateja kupata huduma katika mazingira yaliyo bora wakati wa majira yote ya mwaka.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, inayofanya ziara ya siku mbili ya ukaguzi wa utekelezaji wa ilani, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Ndg. Said Majaliwa amesema Halmashauri yake imesikia kilio cha wafanyabiashara hao, ambao aliwatembelea wiki iliyopita na kuagiza wataalam kufanya tathmini ya kuondoa kero hizo, ambapo makisio ya Tsh. 18,192,600.00 yamewasilishwa ili kuondoa changamoto za soko hilo wakati wakisubiri ufadhili wa ujenzi wa soko la kisasa katika eneo hilo.
"Hatuwezi kuwaacha wafanyabiashara wetu hawa wakae na kufanya biashara zao katika mazingira magumu, kwa kusubiri fedha za ufadhili wa ujenzi wa soko. Tutaendelea kuwaboreshea mazingira yao" Amesema Majaliwa.
Mradi wa ujenzi wa soko la kisasa la Mgandini upo kwenye mpango wa kuidhinishwa kwa awamu ya pili ambao unakadiriwa kugharimu kiasi cha zaidi ya shilling billioni 30 katika mradi wa Green and Smart Cities.
Kamati hiyo ya Siasa Mkoa iliyoongozwa na Katibu wa CCM Mkoa, Ndg. Selemani Sankwa, ilitembelea Makazi ya Wazee wasiojiweza Mwanzange yaliyopo Kata ya Duga, ambapo walielezwa kuwa kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia Wazee 34, kwa sasa kina wazee 15 (Kiume 10, kike 5) na kwamba kinakabiliwa na upungufu wa watumishi hasa kada ya upishi, uchakavu wa majengo na mfumo wa umeme.
Katika eneo la Hospitali ya Wilaya, Kamati ilifahamishwa kuwa huduma zote za msingi zinatolewa Hospitalini hapo, ikiwa ni pamoja na huduma za mama na mtoto, picha na mionzi, kinywa na meno, macho na nyinginezo, huku ukarabati wa chumba cha upasuaji uzazi pingamizi (Maternity theater) ukikamilika tayari kwa matumizi.
Hospital ya Jiji la Tanga ilianza kujengwa mwaka 2018 kama Hospital ya Wilaya ambapo kwa awamu ya kwanza yalijengwa majengo saba ambayo ujenzi wake umekamilika na kuanza kutoa huduma mbalimbali, huku awamu ya pili zikijengwa wodi tatu ambazo ziko hatua ya umaliziaji, mradi huo ukitumia zaidi ya shillingi billioni 1.9, Halmashauri ikitegemea kutumia shillingi million 160 kwa nusu ya mwaka huu wa fedha kukamilisha wodi ya watoto na wanaume.
Ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa itaendelea katika siku yake ya pili kwa kutembelea jengo la kitega uchumi Kange na maeneo ya kutolea huduma za afya katika kata ya Pongwe.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.