Na: Mussa Labani
Julai 10, 2024.
Shule ya Msingi Maweni, iliyopo Kata ya Maweni, imepokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka kwa Shule rafiki ya Hanley Castle, ya nchini Uingereza, ambapo urafiki kati ya shule hizi umedumu kwa kipindi cha miaka kumi sasa.
Vifaa hivyo vimepokelewa siku ya Jumanne, Julai 09, 2024, na Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Dkt. Frederick Sagamiko, katika chumba cha darasa ambacho ujenzi wake ni zao la urafiki huo.
Vifaa vilivyopokelewa ni pamoja na projector mbili, mashine moja ya cherehani, kompyuta moja ya mpakato (laptop), madaftari dazeni tisa, Kalamu za wino dazeni tisa, viatu pamoja na nguo kwa ajili ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Marafiki hao pia wamekubali kutoa kiasi cha shilling milioni 50 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu pamoja na choo.
Shule ya Hanley castle, ambayo ni moja ya shule za Serikali nchini Uingereza, imeahidi kuwapatia uji na chakula cha mchana kinachopikwa shuleni watoto 50 walio yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, kwa kipindi chote cha uwepo wao shuleni hapo.
Mashirikiano hayo pia yamehusisha safari za kubadilishana uzoefu kati ya walimu wa shule ya Maweni na walimu toka Hanley castle ambazo zimekuwa zikifanyika kila mwaka.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.