Halmashauri ya Jiji la Tanga imetenga kiasi cha shillingi million 250 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule mpya ya awali na msingi ya mchepuo wa Kiingereza katika Kata ya Maweni, ambapo kiasi hicho cha fedha tayari kimekwisha ingizwa katika akaunti ya Shule ya Msingi ya Saruji, ambayo ni shule jirani, kwa ajili ya kusimamia ujenzi wa shule hiyo mpya.
Akizungumza na Tanga Television, wakati wa ziara ya Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mohamed Mfundo amesema shule hiyo inajengwa katika eneo hilo ikiwa pia ni namna ya kupanua huduma katika Jiji la Tanga.
Amesema Jiji la Tanga linatakiwa kutanuka, na ujenzi wa majengo yote kuwa mjini, kunalifinya Jiji, hivyo ni lazima huduma zingine ziende pembezoni mwa mji.
"Tuna Shule kama hizi za English medium mbili katika Halmashauri yetu. Tuna mpango katika bajeti hii tuongeze moja, na bajeti ijayo tumepanga tupate zingine mbili, at least zifike shule tano za English medium ambazo zitakuwa chini ya Halmashauri yetu ya Jiji." Amesema Mfundo.
Kamati ya Uchumi, Afya na Elimu pia ilitembelea eneo la Shule ya Sekondari MACECHU iliyopo Kata ya Chumbageni kuona na kuchukua hatua za kudhibiti mmomonyoko wa udongo katika mfereji wa maji ya mvua unaopita karibu na ukuta wa jengo la madarasa na kutishia uimara wa jengo hilo.
Kamati pia ilitembelea eneo la Kange karibu na stendi kuu ya mabasi, panapojengwa soko la wafanyabiashara wadogo-wadogo (Wamachinga) kukagua utekelezaji wa mradi huo.
Wakiwa katika mradi huo, Mchumi wa Jiji la Tanga, Bw. Vedastus Mzee aliiambia kamati kuwa, mradi huo unaojengwa kwa awamu, utakapo kamilika utagharimu kiasi cha zaidi ya shillingi Billion 7, na mpaka sasa tayari umetumia kiasi cha zaidi ya shillingi million 600, kati ya hizo shillingi million 540 ni fedha za kutoka Serikali Kuu, huku Halmashauri ikitenga fedha kutoka mapato ya ndani shillingi million 400 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.