Na: Mussa Labani, Tanga.
Juni 28, 2024.
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga (RAS), Ndg. Pili Mnyema, amewataka Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini wa Mkoa wa Tanga, kutumia dhamana waliyopewa katika kusimamia Vitengo vya Mawasiliano Serikalini kwa kutoa taarifa sahihi kwa jamii juu ya shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali, ili kuondoa taarifa za uzushi.
Mnyema amesema, jamii ikipata taarifa sahihi, taarifa za uzushi hazitaweza kusambaa na kuipotosha jamii. Amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeleta fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ili kutatua kero za wananchi. Amesema ni vizuri jamii ikafahamu kazi kubwa inayofanywa na Serikali yao, na hivyo Maafisa Habari wana wajibu wa kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo.
RAS Mnyema amesema hayo wakati akiwapongeza Wakuu wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano Serikalini, katika Mkoa wa Tanga vilivyopata tuzo katika utoaji wa taarifa za kazi za Serikali, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kufuatia tathmini iliyofanywa na Wizara ya Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kuangalia namna Wizara, Taasisi, Ofisi za Mikoa na Halmashauri zinavyotoa taarifa kwa umma kwa kipindi cha mwaka 2023/2024.
Akizungumzia umuhimu wa vitendea kazi kwa Vitengo hivyo, Mnyema amesema, kufuatia mabadiliko makubwa katika teknolojia ya habari, ipo haja ya Vitengo kupatiwa vifaa vya kisasa ili watendaji wake waweze kufanya vizuri zaidi.
"Kwa Mkurugenzi hapa (Mkurugenzi wa Jiji la Tanga), sasa ni fursa kwako, kuhakikisha kwamba, tunaimarisha Kitengo chetu cha Mawasiliano kwa kuwapatia vifaa vya kisasa, lakini pia na kuwawezesha masuala ya usafiri kwenda kuzunguuka kwenye miradi, najua Halmashauri ya Jiji tuna miradi mingi sana ambayo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuletea fedha za kutosha, kwa hiyo tuna kazi kubwa ya kuhabarisha umma nini kimefanyika katika kipindi cha awamu ya Sita ya Serikali" Amesema RAS Mnyema.
Vitengo vya Mawasiliano Serikalini vilivyopata tuzo ni kutoka Halmashauri ya Jiji la Tanga, ambayo ilishika nafasi ya tisa (9) kati ya 184, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ya tisa (9) kati ya 26 na Tanga UWASA ya sita (6) kati ya 84.
Tathmini hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya kuimarisha mawasiliano ya Serikali kwa umma, lengo likiwa ni kuwafanya Maafisa Habari kutoa taarifa kwa kina kwa wananchi kuhusu miradi yote ya maendeleo.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.