Programu ya Tanga Yetu inayotekelezwa katika Jiji la Tanga kwa ufadhili wa Fondation Botnar (Shirika la kimaendeleo la Uswis), Julai 01, 2025, imezindua miradi saba ya awamu ya pili ya utekelezaji wake, yenye thamani ya zaidi ya shillingi billioni 2.4, yenye lengo la kukuza mabadiliko chanya katika jamii na kuongeza ushiriki wa vijana katika kujiletea maendeleo yao, ikiwa sasa inafanya jumla ya miradi hiyo kufikia 11, baada ya miradi mingine minne ya zaidi ya shillingi billion 1.2, kuzinduliwa Mei 16, 2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa miradi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Dadi Kolimba, amepongeza wafadhili wa programu ya Tanga Yetu, Taasisi ya Fondation Botnar na washauri na meneja wa fedha wa miradi, Taasisi ya Innovex, kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo, ambapo amewataka walengwa kuweka umakini na kujipanga tangu mwanzo ili miradi iwe na uendelevu.
Amesema idadi ya vijana wanaomaliza vyuo vya kati na vikuu, ni kubwa sana, na soko la ajira ni dogo sana, hivyo miradi hii itasaidi kuwainua vijana kujiajiri na kuajiri vijana wenzao, na hivyo kutimiza lengo la kulifanya Jiji la Tanga kuwa sehemu rafiki kwa watoto na vijana.
Awali, akitoa historia fupi ya programu ya Tanga Yetu Initiative, Mwakilishi wa Fondation Botnar Dkt. Hassan Mshinda, amesema programu hiyo yenye lengo la kuboresha maisha ya vijana katika nchi zinazoendelea, katika awamu ya kwanza ilifanya miradi iliyolenga maeneo matatu ya kuimarisha huduma za afya na elimu, Ujasiriamali, na kulijengea uwezo Jiji la Tanga katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa programu ya Tanga Yetu, Bw. Juma Rashid Iddi, ameitaja miradi saba iliyozinduliwa kuwa, miradi ya afya ni mitatu, michezo mmoja, ujasiriamali mmoja, vijana mmoja, malezi na makuzi mmoja.
Miradi hiyo 11 iliyozinduliwa, ni kati ya 18 itakayotekelezwa katika kipindi kisichopungua miezi 21 kwa mwaka 2025 hadi 2027, ambayo imewalenga vijana katika jiji la Tanga ambao kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 idadi ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ni 155,097 sawa na asilimia 39.4 ya wakazi wa Jiji la Tanga.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.