Juni 10, 2023.
Mwenge wa Uhuru 2023 umemaliza mbio zake katika Wilaya ya Tanga baada ya kukimbizwa umbali wa kilomita 119 kuanzia eneo la mapokezi, Uwanja wa Ndege wa Tanga, hadi kijiji cha Kimang'a Wilayani Pangani ambapo Mwenge huo umekabidhiwa kwa Wilaya ya Pangani.
Akitoa salamu fupi za kuagana katika eneo la makabidhiano, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa kwa Mwaka 2023, Ndugu Abdallah Shaib Kaimu amesifu utekelezaji na usimamizi mzuri wa miradi iliyopitiwa na Mwenge katika Wilaya ya Tanga.
Ndugu Kaimu amesema Mwenge wa Uhuru 2023 umeridhishwa na ubora wa miradi na uhifadhi wa nyaraka zote muhimu katika utekelezaji wa miradi, ambayo Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikileta fedha nyingi kuitekeleza, ili kusaidia kuondoa kero kwa wananchi, na hivyo amewataka viongozi wa Wilaya ya Tanga kuendelea kumsaidia Rais kwa kutekeleza miradi hiyo kwa viwango vinavyostahili, huku akisifu ushirikiano mzuri kati ya Chama na Serikali Wilayani Tanga.
Kiongozi huyo pia alitumia muda huo kwa kutoa pole kwa majeruhi wa ajali ya gari iliyokuwa kwenye msafara wa Mbio za Mwenge, na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie uponyaji wa haraka.
Gari iliyopata ajali ilikuwa moja kati ya gari za matangazo na hamasa, wakati ikitangulia Kijiji cha Kimang'a Wilayani Pangani kwenye eneo la makabidhiano ikiwa na MC, Dj's, Wachekeshaji na Maafisa wengine wa Halmashauri, ilipata ajali umbali mfupi kutoka eneo la Kigombe, ambapo majeruhi walipelekwa Kituo cha Afya Kimang'a kwa huduma ya kwanza na baadae kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo.
Awali, akitoa taarifa ya Mbio za Mwenge Wilayani Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Ndg. Hashim Mgandilwa amesema Mwenge umepita katika miradi saba yenye thamani ya shillingi Billion 2.736, ambapo kati ya miradi hiyo, miradi minne imefunguliwa, miwili imetembelewe na mmoja kuwekewa jiwe la msingi.
Akizungumzia mkesha uliofanyika Shule ya Msingi Gofu Juu, Mgandilwa amesema katika mkesha huo, kumefanyika zoezi la utoaji wa chanjo ya Uviko - 19 ambapo watu 102 walichanja, upimaji wa VVU/UKIMWI na uchangiaji wa damu ambapo unit 14 za damu zilipatikana.
Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 inasema “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa”. Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu ni Mkoani Manyara Oktoba 14, 2023.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.