Juni 09, 2023.
Mwenge wa Uhuru umewasili Mkoani Tanga ukitokea Kusini Pemba na kupokewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba, katika Uwanja wa Ndege wa Tanga, tayari kuanza mbio za siku kumi na moja katika Halmashauri zote za Mkoa huu.
Mwenge wa Uhuru umeingia Mkoani Tanga ikiwa ni Mkoa wa kumi na nne tangu kuzinduliwa kwa mbio za mwaka huu April 2, 2023 Mkoani Mtwara na utakamilisha ratiba yake ya Mkoa ifikapo Juni 19 na kukabidhiwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro Juni 20.
Mwenge wa Uhuru ambao kwa mwaka huu unaongozwa na Ndugu Abdallah Shaib Kaimu, utaanza mbio zake Mkoani Tanga kwa kukimbizwa katika Wilaya ya Tanga ambapo utakagua, kuweka mawe ya msingi na ufunguzi wa miradi saba yenye thamani ya shillingi Billioni 2.7 ikiwemo ya umma na binafsi.
Miradi hiyo itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Tanga ni pamoja na mradi wa vijana Tumbilini, uzinduzi wa kisima cha maji Mwahako, uzinduzi wa Kituo cha mafuta cha Shehoza Magaoni, Shule ya Msingi Mnyanjani ufunguzi wa vyumba vya madarasa, ufunguzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika hospital ya Safi Medics, uzinduzi wa barabara ya Askari na Lumumba kata ya Ngamiani kaskazini na chanzo cha maji Mabayani ikiwa ni pamoja na zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Pande.
Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 inasema “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa”. Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu ni Mkoani Manyara Oktoba 14, 2023.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.