Juni 13, 2025.
Mwenge wa Uhuru 2025 unatarajiwa kupokelewa Wilayani Tanga siku ya Jumatatu, Juni 16, 2025, katika uwanja wa shule ya msingi Mabambani, iliyopo mtaa wa Mpirani, kata ya Chongoleani, ukitokea Wilaya ya Mkinga, na kukimbizwa katika mitaa 43 ya Jiji la Tanga, ambapo utakagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua jumla ya miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya shillingi 3,058,289,671.99
Akitoa taarifa ya ujio wa Mwenge wa Uhuru kwa waandishi wa habari, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba, amesema miradi itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru ni ujenzi wa madarasa manne ya ghorofa la chini, matundu 13 ya vyoo na ofisi ya walimu katika shule ya msingi Mbuyuni. Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya awali shule ya msingi Mwakidila.
Miradi mingine ni ufunguzi wa ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Tongoni, ufunguzi wa barabara ya Sahare yenye urefu wa mita 600 iliyojengwa kiwango cha lami, ufunguzi wa jengo la X-Ray kituo cha Afya Makorora, mradi wa ufungaji wa dira za maji za malipo ya kabla, na mradi wa kikundi cha vijana cha kutengeneza gypsum, wakiwa ni wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mhe. Kolimba amesema shughuli ya mkesha wa Mwenge wa Uhuru itafanyika katika uwanja wa shule ya msingi Kisosora, kata ya Chumbageni, ambapo mabanda ya maonesho na burudani kutoka kwa wasanii waalikwa mbalimbali zitakuwepo, na hivyo amewasihi wakazi wa Tanga kujitokeza kwa wingi katika eneo la mapokezi, njia itakayopita Mwenge wa Uhuru, na katika eneo la mkesha.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu inasema, "Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu"
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.