Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Jiji, Dkt. Frederick Sagamiko, leo Jumanne, Julai 09, 2024, imekutana na wataalamu kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Chuo cha Mipango Mwanza (IRDP), na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambao kwa pamoja wanatekeleza mradi wa "Bahari Maisha" chini ya ufadhili wa UNDP, wenye lengo la kuongeza thamani kwenye mazao ya bahari.
Mradi wa Bahari Maisha unakusudiwa kutekelezwa katika Jiji la Tanga kwa kuviwezesha vikundi vya wakulima wa mwani, wafugaji wa jongoo bahari, kaa, na mazao mengine ya bahari na udhibiti wa taka/masali kutoka kwa mazao hayo, ambapo tayari UNDP imeidhinisha fedha za mradi huo, kwa Jiji la Tanga.
Shughuli zinazotegemewa kufanyika ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha bidhaa kwa mazao ya bahari, utoaji wa elimu kujua thamani ya mazao hayo, kuwafundisha kwa vitendo utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na mwani, uongezaji thamani wa bidhaa za mwani, na utunzaji wa mazingira kwa kuepuka matumizi ya kemikali katika kazi zao.
Mradi pia umelenga kuwawezesha kiuchumi vijana, ambapo utatoa nafasi kwa baadhi ya vijana wa eneo la mradi kushiriki katika utekelezaji wa mradi chini ya UNDP.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.