Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Hashim Mgandilwa, leo Jumatano, Mei 10, 2023, ameongoza kikao cha tathmini ya Mkataba wa Lishe, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Ofisi Kuu ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, chenye lengo la kupokea na kupitia utekelezaji wa Tathmini ya Hali ya Lishe kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Akifungua kikao hicho, Mhe. Mgandilwa amewataka wajumbe wa kikao hicho kufahamu kuwa lishe ndio msingi wa kila kitu, na kwamba kikao hicho ni muhimu katika uboreshaji wa lishe katika jamii, ili kuondokana na udumavu.
Mgandilwa amewataka Maafisa Watendaji wa Kata kuyatekeleza yanayoamuliwa katika vikao, na kutumia vikao na mikutano katika maeneo yao kwa kutoa elimu, ikiwa ni pamoja na kuwaalika Maafisa Lishe katika Kata zao, ili jamii ifahamu umuhimu wa lishe bora, hususan siku 1000 za mwanzo za mtoto, na kuondokana na fikra potofu za lishe bora ni chakula cha "mboga saba".
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Dkt. Sipora Liana amewataka Watendaji wa Kata kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa afua za lishe, ili kujiepusha na kutia doa hatua nzuri ya hali ya lishe katika Jiji la Tanga.
Awali, Kaimu Afisa Lishe Jiji la Tanga, Ally Kassembo, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji ya tathmini ya Lishe katika robo ya tatu (Januari - Machi) kwa mwaka wa fedha 2022/2023, ambapo katika taarifa hiyo, amevitaja vituo vya afya vya Ngamiani, Mikanjuni, Duga, Makorora, Pongwe na Hospital ya Wilaya kuendelea kutoa matibabu ya utapiamlo ya asili (local treatment) kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Kikao hicho cha tathmini ya Mkataba wa lishe, kimehudhuriwa na baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo vya Halmashauri, Maafisa Watendaji Kata na wadau wengine wa lishe katika Jiji la Tanga.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.