November 20, 2023.
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Ndg. Said Majaliwa amewataka Watendaji ngazi ya Kata na Mitaa katika jiji la Tanga, kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, kusikiliza kero za wananchi na kukusanya mapato ya Serikali, huku akitoa onyo kwa wale wanaochelewa kufika kazini.
Mkurugenzi Majaliwa ameyasema hayo wakati alipokuwa akiongea na Watendaji wa Serikali katika Kata za Kirare na Marungu, ikiwa ni muendelezo wa utaratibu aliojiwekea wa kupita katika Kata zote za Jiji la Tanga, ili kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wakazi na watumishi wa maeneo hayo.
Mkurugenzi Majaliwa ametumia vikao hivyo kusisitiza watumishi kufanya kazi kwa pamoja (team work), kwa kushirikisha Idara na sekta zingine ili kukamilisha mradi kwa wakati, huku akiwataka watendaji hao, kutomficha mtu anayekwamisha utekelezaji wa miradi kwani hayuko tayari kumvumilia mtu mzembe.
Akizungumzia usikilizaji wa kero za wananchi, Majaliwa amewataka Watendaji wa Kata kuwa na daftari la kuorodhesha kero walizosikiliza na utatuzi waliochukua, na kujenga utaratibu wa kupita katika shule na vituo vya kutolea huduma za afya kufuatilia iwapo watumishi wa umma katika eneo hilo wanawahi na kusalia katika maeneo yao ya kazi kuwahudumia wananchi.
Akiwa katika Kata ya Marungu, Majaliwa ameonyesha kutokufurahishwa na taarifa za uwepo wa fedha katika akaunti ya Kata, huku utekelezaji wa miradi ukiwa ni wa kusuasua, na hivyo kumuagiza Afisa Utumishi kumuondoa Mtendaji wa Kata ya Marungu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.
Maagizo hayo ni baada ya kukuta zaid ya Mil 40 za ujenzi wa madarasa 2 na ofisi zikiwa katika akaunti ya kata tangu 28.6.2023, na kuonya kuwa iwapo atakuta fedha kwenye akaunti ya mradi zimekaa bila maelezo, atachukua hatua kwa mhusika.
Mkurugenzi Majaliwa amesisitiza suala la ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa leseni za biashara kwenye mitaa, na kuhimiza usafi wa mazingira kwenye maeneo ya makazi.4
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.