Januari 29, 2025.
Mkutano wa Baraza la Madiwani wa kupokea taarifa za utekelezaji kutoka katika kata, umefanyika leo, jumatano, Januari 29, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi kuu ya Halmashauri, ikiwa ni utangulizi wa mkutano wa baraza wa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025, utakaofanyika kesho, alhamisi Januari 30, 2025.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi na umaliziaji wa miradi viporo katika ngazi ya kata, Mwenyekiti wa mkutano huo, ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Abdulrahman Shiloow, amempongeza Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini na Menejimenti yake kwa jitihada mbalimbali walizochukua kuhakikisha kazi ya ujenzi wa miradi inafanyika, sambamba na umaliziaji wa miradi viporo.
Amesema amekuwa akifuatilia taarifa za utekelezaji kutoka kila kata, na kuona kinachofanyika katika maeneo hayo, na hivyo kuwataka Watendaji wa Halmashauri kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati ili kuweza kutoa huduma iliyokusudiwa.
Aidha, ameitaka Idara inayosimamia utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kurahisisha taratibu za utoaji wa fedha kwa vikundi hivyo, ili waanze kuzitumia. Amesema dirisha jingine la mikopo limefunguliwa na kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kitakopeshwa.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tanga, Meja (Mstaafu) Hamisi Mkoba, akizungumza katika mkutano huo, amepongeza utekelezaji wa miradi na ushirikiano uliopo kati ya Chama na Watendaji, akihimiza kila mmoja kutekeleza wajibu wake kwa manufaa ya Jiji la Tanga.
Baraza la Madiwani la kupokea taarifa za kata hufanyika kila robo ya mwaka wa fedha, ambapo Madiwani huwasilisha taarifa za utekelezaji kutoka kwenye kata zao, kwa kipindi cha miezi mitatu.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.