Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, ambaye pia ni Waziri wa Afya wa Tanzania, Mhe. Ummy A. Mwalimu, amewakaribisha wakazi wote wa Mkoa wa Tanga kujitokeza kupata huduma ya upimaji wa afya katika kambi maalum ya upimaji wa afya iliyoandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Afya Check, Ofisi ya Mbunge wa Tanga Mjini na Halmashauri ya Jiji la Tanga, itakayoanza tarehe 21 hadi 25 mwezi huu wa Augosti, 2023, katika Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Usagara, Jijini Tanga.
Mheshimiwa Waziri Ummy ametoa ukaribisho huo wakati akitangaza rasmi ujio wa kambi hiyo katika Jiji na Mkoa wa Tanga ambapo amesema huduma zitakuwa wazi kwa wakazi wote wa Mkoa wa Tanga na kwamba hakuna malipo ya kiingilio wala kujiandikisha, na kwamba itakuwa ni bure kwa wote.
Mheshimiwa Ummy amesema ni vizuri kuwa na utaratibu wa kupima afya kuliko kusubiri mpaka mtu aumwe ndio anakwenda hospitali, na kwamba yapo magonjwa ambayo yakigundulika mapema, upo uwezekano wa kujinasua kwenye tatizo hilo.
"Na kubwa, unaweza, wala usifanye mambo mengi. Unaweza ukafanya mambo kama matatu tu, tunasema 'know your numbers', jua namba zako.
Namba zako ya kwanza, uzito wako. Namba ya pili kuhusu kisukari. Kwa sababu kisukari ndio kinakuja kupelekea magonjwa kama shinikizo la damu, changamoto za moyo, figo, n.k. Na namba ya tatu ni BP, shinikizo la juu la damu" Amesema Waziri Ummy.
Akizungumzia mambo yatakayofanyiwa upimaji, amesema kwa upande wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yatakayo fanyiwa upimaji ni pressure (shinikizo la damu), Kisukari, Saratani (aina tatu: mlango wa kizazi, matiti na tezi dume), na macho.
Na kwa magonjwa yanayo ambukiza, ameyataja magonjwa ya UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria, na iwapo mtu akigundulika na ugonjwa, atapatiwa dawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Afya Check, Dr. Isaac Maro ameshauri jamii kujenga utamaduni wa kupima afya japo mara moja kwa mwaka.
Amesema upimaji wa afya sio jambo la gharama kubwa kulinganisha na matumizi yetu ya kila siku, na kwamba kama vile tunavyofanya service ya magari na baiskeli zetu, ni muhimu pia kuangalia afya zetu na kuzilinda.
Huduma kwa kambi ya upimaji wa afya zitatolewa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 alasiri kwa siku tano za upimaji.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.