Na. Mussa Labani, Tanga.
Julai 18, 2024.
Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, imewapongeza wakazi wa Mtaa wa Mbugani, Kata ya Masiwani kwa kutoa ekari 16 kwa huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Msingi katika eneo hilo.
Pongezi hizo zimetolewa leo, alhamisi Julai 18, 2024, na Kamati hiyo ilipotembelea shule ya msingi Mbugani, iliyojengwa kwa msaada wa taasisi ya Islamic Help, wakati kamati ilipokuwa katika ziara yake ya kawaida ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Kamati pia imempongeza Diwani wa Kata ya Masiwani, Mhe. Longson David Njau, Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi ya Kata, na wafadhili waliosaidia ujenzi wa shule hiyo ya msingi, Taasisi ya Islamic Help, ambayo imesaidia ujenzi wa vyumba saba vya madarasa, matundu sita ya vyoo, jengo la utawala, na kisima cha maji.
Akiongea kwa niaba ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati, ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Abdulrahman Shiloow, ameitaka Halmashauri kuhakikisha inakamilisha usajili wa shule, uwekaji wa samani (madawati, viti na meza), pamoja na mgao wa walimu ili ifikapo Januari 2025, shule ianze kufanya kazi.
Kwa upande wao wakazi wa mtaa huo, wameiomba Kamati ya Fedha na Uongozi kuwasaidia kupata barabara ya kufika shuleni hapo ili watoto watakapoanza shule, wasipate shida ya jinsi ya kufika.
Mbali na kutembelea shule hiyo, Kamati pia ilitembelea na kukagua mazingira ya vituo vya kulelea watoto/malezi ya watoto wadogo (Day Care Centre), pamoja na Kituo cha Afya Mafuriko (Kihongwe Hospital), ambapo Kamati iliitaka Halmashauri kuangalia namna ya kukamilisha jengo la huduma ya mama na mtoto.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.