Na. Mussa Labani, Tanga.
Juni 27, 2024.
Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Tanga, ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Abdulrahman Shiloow, umepitisha Rasimu ya Sheria ndogo za Halmashauri ya Jiji la Tanga za mwaka 2024, baada ya kuzijadili na kutoa mapendekezo ya maboresho kwa rasimu hiyo, ambapo zitakapo kamilika, zitafuta sheria ndogo zinazotumika sasa za mwaka 2014 na 2019.
Akifungua mkutano huo, Mstahiki Shiloow amesema, rasimu hiyo ni nyongeza ya vitu vidogo vidogo vilivyoongezwa kwenye sheria zinazotumika sasa, ambapo maboresho hayo yamefanywa ili kuendana na wakati, kuwezesha Halmashauri kutimiza wajibu wake wa kuihudumia jamii.
Akiwasilisha rasimu hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Kaimu Mwanasheria wa Jiji la Tanga, Idrisa Mbondera, amesema utungaji wa sheria ndogo hizo umefuata utaratibu wa kisheria kama ulivyoainishwa kwenye kifungu cha 90 cha Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288.
Amesema mchakato huo umepita katika hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutolewa kwa tangazo la kusudio la kutungwa sheria ndogo ili wananchi na wadau waweze kutoa maoni au pingamizi.
Rasimu hiyo pia imepita katika vikao vya maendeleo vya kata (WDC), na kujadiliwa katika vikao mbalimbali vya Halmashauri.
Jumla ya sheria ndogo tisa ziliwasilishwa ambazo ni Sheria ndogo za ada na ushuru, sheria ndogo za ada za burudani, sheria ndogo za ushuru wa mazao ya uvuvi, sheria ndogo za ushuru wa nyumba za kulala wageni, sheria ndogo za ushuru wa masoko, minada na magulio, sheria ndogo ya Afya, udhibiti wa taka ngumu na mazingira, na sheria ndogo ya ushuru wa huduma.
Sheria ndogo nyingine ni ya ushuru wa maegesho na vituo vya mabasi, na sheria ndogo ya ada ya leseni ya shughuli za biashara.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.