Kamati ya lishe ya Jiji la Tanga, leo, Jumanne, Mei 9, 2023, imekutana katika kikao cha kawaida cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/2023, chini ya Mwenyekiti wake, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Dkt. Sipora Liana kwa lengo la kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka.
Akiwasilisha taarifa ya Kitengo cha Lishe, Kaimu Afisa Lishe Jiji la Tanga, Bw. Ally Kassembo, amesema Jiji limeendelea kufanya vizuri katika kipimo cha kadi ya alama kutoka kwenye kata, ngazi ya Halmashauri na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Afisa Lishe Kassembo ameyataja baadhi ya mafanikio katika robo ya tatu kuwa ni pamoja na Halmashauri kuendelea kununua bidhaa kwa ajili ya matibabu ya utapia mlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5, na vituo vya kutolea huduma za afya kutumia vyanzo vya fedha za NHIF, User fee, Basket Fund na CHF kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za lishe.
Awali akifungua kikao, Mkurugenzi Dkt. Liana amewataka wajumbe wa kikao hicho, ambacho huhusisha baadhi ya Wataalam wa Halmashauri na wadau kutoka taasisi zingine, kufanya vizuri katika utekelezaji wa shughuli za lishe, huku akisifu utendaji kazi mzuri wa aliyekuwa Mkuu wa Kitengo hicho, Bi. Sakina Mustafa, ambaye kwa sasa amepangiwa kituo kingine cha kazi.
Mbali na Idara za Halmashauri, wadau wengine waliowasilisha taarifa zao za utekelezaji ni PASADIT OVC Project, chini ya Mradi wa USAID Kizazi Hodari, na Shirika lisilo la Kiserikali la Centre Against Gender Based Violence (CAGBV) Tanga.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.