Katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabia ya nchi, Jamii wilayani Tanga, Imetakiwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali kama Shule, hospital na vyanzo vya maji ili kutunza mazingira.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wilaya ya Tanga Mikaya Dalmia wakati wa zoezi la upandaji miti katika Zahanati ya kisimatui kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Uhuru wa miaka 61 ya Tanzania Bara.
Katibu Tawala amesema wameona ni vyema katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Uhuru, kufanya shughuli za kijamii kwa kutunza mazingira kwenye Zahanati ya Kisimatui kwa kupanda Miti, Usafi wa Mazingira ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia ya nchi.
Dalmia ameongeza kuwa upandaji wa Miti katika zahanati hiyo itawasaidia Zaidi wagonjwa wanaofika kupata huduma za kiafya kupumzika katika maeneo hayo .
Pia amesema Utunzaji wa Mazingira ni jukumu la kila mwananchi katika kuhakikisha wanatunza kwa kupanda miti, usafi wa mazingira ambapo itasaidia hata vyanzo vya maji katika matumizi mbalimbali ya kibinadamu pamoja na uzalishaji wa kiuchumi.
Aidha amesema wananchi wamekuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira ambapo viwanda mbalimbali kama Saruji vimepanda miti ya kutosha hali inayoonesha mkoa wa Tanga ni Kinara katika utunzaji wa mazingira.
Pia Katibu Tawala amewasisitiza wananchi kupitia Afisa Mazingira Jiji la Tanga kutoa miche ya bure itakayowawezesha kupanda katika maeneo yao lengo likiwa ni kuhakikisha wanatunza mazingira kwa ajili ya Taifa la baadae na sasa.
Nae Afisa Misitu Jiji la Tanga Maajabu Mohammed amesema baada ya zoezi la upandaji Miti katika eneo la zahanati ya Kisimatui, kila mwananchi ataondoka na miche itayowawezesha kupanda katika makazi yao huku akiwasisitiza kuilinda ili iweze kuleta tija hapo baadae.
Kwa upande wake Afisa Maliasili Jiji la Tanga Aneny Nyirenda amewahimiza wananchi kupanda Miti na shughuli nyingine za Mazingira pamoja na Afya kama ufanyaji wa mazoezi ili kubeba taswira ya uhuru katika Taifa
Kwa Upande wao wananchi wa Mgwisha pamoja na Kisimatui wakaishukuru serikali kwa ugawaji wa miche hiyo huku wakiahidi kuitunza ili iwaletee manufaa hapo baadae.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.