Mbunge wa Jimbo la Tangamjini, Madiwani na Watendaji wa Kata na Wataalamu wa Jiji la Tanga leo wametembelea chanzo cha maji eneo la Mabayani na Mtambo wa kusafisha maji mowe uliopo kata ya Kiomoni, ziara hiyo iliyoandaliwa na TANGAUWASA imelenga kuwapa uelewa wawakilishi wa wananchi kuhusu utendaji kazi wa Mamlaka, bei ya huduma za maji pamoja na kutatua changamoto zilizopo na kupokea ushauri kwa manufaa ya watumiaji huduma hiyo.
Katika ziara hiyo Mbunge wa jimbo la Tangamjini ambaye pia ni Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Ummy Mwalimu amewataka TangaUwasa kusambaza maji katika maeneo ya pembezoni mwa Jiji kama Chongoleani,Ndaoya,Mpirani,Kibafuta na Mleni ili kuhakikisha Wananchi wa maeneo hayo wanapata maji safi na salama kwani huduma ya maji ni muhimu katika maisha.
“Suala la huduma za maji kwa Wananchi wangu wa jiji la Tanga ni moja kati ya Vipaumbele vyangu muhimu nitahakikisha linapata ufumbuzi wa kudumu hususani bei za bili za maji” alisisitiza Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mhe.Ummy Mwalimu
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Abdrahaman Shilow amesema kuwa wanaishukuru mamlaka ya maji TANGAUWASA kwa kuwapatia fursa ya kutembelea na kufahamu namna uzalishaji maji unavyofanyika huku akigusia suala zima la bei kubwa za bili za maji kwani imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa jiji hili ambayo inahitajika kutatuliwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TangaUwasa mhandisi Geofrey Hilly amewahakikishia Mbunge waheshimiwa madiwani pamoja na kuwa kero ya bili ya maji inashughulikiwa pamoja na marekebisho ya mita za maji, pia ameongeza kuwa wapo katika mchakato wa kupitia bei mpya za maji.
TANGAUWASA ni Mamlaka ya Maji inayohudumia Wananchi zaidi ya 200,000 wa Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.