Na: Emma Kigombe
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mheshimiwa Omary Mgumba amefanya ziara Katika kata ya Chongoleani Jijini Tanga siku ya Jumanne, Augosti 9, 2022 yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zilizopo katika eneo hilo. Ziara hii ambayo alianzia kwa kutembelea Bandari ya Tanga, ni ya kwanza kufanya ndani ya Jiji la Tanga tangu ahamishiwe Mkoani Tanga akitokea Mkoa wa Songwe, siku tatu zilizopita.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Chongoleani, Mgumba amewapongeza wakazi hao kwa kupata mradi mkubwa wa bomba la mafuta katika kata yao ambao utagharimu takribani trillion 8 ambapo manufaa yake yameshaanza kuonekana katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mgumba amesema kuwa Chongoleani ni eneo muhimu kwa uchumi wa taifa kutokana na mradi wa bomba la mafuta na hivyo wananchi wa kata hiyo ni muhimu sana katika ulinzi wa mradi huo.
"kata yenu hii kitaifa ndio iliyopata mradi mkubwa kuliko zote na manufaa yake mtaanza kuyaona na mengine yameshaanza kuonekana mapato ya Halmashauri ya jiji la Tanga yameanza kupaa maana yake kila fedha inayoongezeka inatupa nguvu serikali kuja kuwahudumia kwa uzuri sana" alisema Mgumba.
Aidha Mgumba amemshukuru Rais Samia kwa namna alivyotekeleza na kutatua shida za wananchi hususani katika kata ya chongoleani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amewataka wananchi wa Chongoleani kuendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wanaoenda kuwekeza katika eneo hilo.
Pia mkuu wa wilaya ya tanga ameyataka makampuni ambayo yameshafanya tathmini kuweza kuwalipa fidia wananchi
" kwenye Uwekezaji huu wa bomba la mafuta kumetokea watu wengi sana wakitaka maeneo kwenye mitaa yetu hii, yapo makampuni ambayo tayari wameshalipa fidia lakini wapo baadhi yao wamefanya uthamini bado fidia hawajalipa " Alisema Mgandilwa
Nae mstahiki meya wa jiji la Tanga Mh. Abdurahman Shiloow ameeleza mikakati ya Halmashauri katika Kuendeleza kata ya chongoleani kuwa mji wa mafuta.
"Siku za mbeleni Halmashauri ya jiji la tanga imepanga kutengeneza kata hii na pembezoni mwake kuwa mji wa mafuta, tumapanga kabisa sasa ndani ya Tanga tuwe na mji wa mafuta na kata hii ndio itakuwa makao makuu ya mji wa mafuta". Alisema Shillow
Pia mstahiki meya aliongeza kwa kusema kuwa wamewekeza katika kata ya chongoleani kwa kuboresha miundombinu ambapo katika mwaka wa fedha uliopita halmashauri imetumia zaidi ya bilioni 194 katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo ambapo katika fedha hizo milioni 80 zimetoka serikali kuu na milioni 114 ni mapato ya ndani ya Halmashauri., na kwa mwaka huu fedha Halmashauri imetenga milioni 208 ambazo zimeshaanza kutumika na zitaenda kujenga madarasa, matundu ya vyoo, bweni, nyumba za walimu shule za msingi na sekondari.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.