Januari 14, 2025.
Kamati ya Uchumi, Afya na Elimu ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Habiba Namalecha, leo Jumanne, Januari 14, 2025, imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya sekta za huduma za jamii, ikiwa ni maandalizi ya kikao cha kamati cha kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa kazi za Halmashauri kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025, kwa Idara na Vitengo vilivyo chini ya Kamati hiyo.
Katika ziara hiyo, kamati ilitembelea miradi miwili ya sekta ya elimu ya msingi na sekondari. Ambapo katika elimu ya awali na msingi, kamati ilitembelea Shule ya Msingi Mwakidila kujionea kazi ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, vyumba vitatu vya ofisi na matundu mawili ya vyoo vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu, vilivyojengwa kwa msaada wa Shirika la Comfort Aid International, ikiwa ni pamoja na madawati 100.
Kamati imepongeza wadau hao kwa msaada ambao umetekelezwa kwa ubora na kwa wakati. Shule ya awali na msingi ya Mwakidila ni moja ya shule zenye idadi kubwa ya wanafunzi, ambapo kwa sasa ina zaidi ya wanafunzi 2000 wanaotoka Kata za Tangasisi na Masiwani.
Kamati ilitembelea kata ya Maweni kukagua kazi ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kasera, inayojengwa nyuma ya chuo cha Utumishi, ambapo kwa mujibu wa mkataba, ujenzi huo unatakiwa kukamilika ifikapo tarehe 18/04/2025.
Mradi huo wa Sekondari ya kutwa, ambao umeingiziwa fedha zaidi ya shillingi million 584, unahusisha ujenzi wa vyumba nane vya madarasa, jengo la utawala, maabara tatu, maktaba, jengo la TEHAMA, vyoo, kichomea taka na tanki la kuhifadhi maji la chini ya ardhi.
Kamati imeridhishwa na kazi, ambapo leo imeshuhudia kazi ya uwekaji wa zege la msingi na tayari misingi ya majengo yote ikiwa imekwisha andaliwa kuwekewa zege.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.