Januari 8, 2025.
KAMATI ya kudhibiti UKIMWI ya Halmashauri ya Jiji la Tanga (CMAC), leo Jumatano Januari 8, 2025, imefanya ziara ya kukagua shughuli za mapambano dhidi ya UKIMWI katika Jiji la Tanga, ikiwa ni ziara yake ya kawaida inayofanyika kila robo ya mwaka, ikiwa ni maandalizi ya kikao cha Kamati kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025, kinachotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Katika ziara hiyo, Kamati iliongozwa na Mwenyekiti wake, Naibu Meya wa Jiji, Mhe. Rehema Mhina, ambapo ilianza kwa zoezi la ugawaji wa vishikwambi 312 kwa walimu wa shule za Msingi na Sekondari, zoezi lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano Ofisi Kuu ya Jiji, na kisha kutembelea Kituo cha Afya Pongwe kuangalia shughuli za huduma za virusi vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI (CTC), na kugawa mipira ya kiume (kondomu) katika maeneo hatarishi katika kata ya Pongwe.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mhe. Mhina amemshukuru Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali afya za wakazi wa Jiji la Tanga, kwa kutoa vishikwambi vyenye mada/masomo maalum kwa wanafunzi juu ya stadi za maisha na afya ya uzazi, kujikinga na virusi vya ukimwi, jinsia na mengine ya kumjenga kijana.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha CTC katika Kituo cha Afya Pongwe, Daktari Ramadhani Juma Kayoga, amesema kitengo hicho kilichoanza huduma mwaka 2009, kwasasa kinahudumia kati ya watu 10 hadi 40 kwa siku, na kinatoa huduma kwa watoto kwa siku za jumamosi.
Akizungumzia mafanikio ya kitengo hicho, Kayoga amesema ni pamoja na Kupunguza idadi ya maambukizi ya VVU, Kupunguza idadi ya maambukizi kutoka kwa mama na mtoto, Kuanzishwa kwa clinic ya watoto siku ya jumamosi na Kutoa nauli na kifungua kinywa kwa watoto ili kuwezesha nauli ya kuudhuria clinic.
Kamati imepongeza uongozi wa kituo na wadau wanaoshirikiana nao, Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Health Promotion Support (THPS), katika jitihada zao za kuelekea zero tatu za hakuna maambukizi mapya, kifo wala unyanyapaa.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.