Na: Mussa Labani, Tanga.
Novemba 9, 2023.
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, imeeleza kuridhishwa kwake na ubora wa miradi na mipango ya ukamilishaji wa miradi katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, baada ya kukamilisha ziara ya siku mbili katika Halmashauri hiyo ya ukaguzi wa utekelezaji wa ilani, ikiwa ni sehemu ya majukumu ya Kamati hiyo kwa mujibu wa Katiba na miongozo ya Chama hicho.
Akizungumza katika hitimisho la siku mbili za ziara hiyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Ndg. Selemani Sankwa, ambaye ndiye aliyeongoza Kamati hiyo, amewapongeza watendaji wa Jiji la Tanga chini ya Mkurugenzi wa Jiji hilo, Bw. Said Majaliwa, kwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Ndg. Rajabu A. Abdallah aliyoyatoa katika ziara yake mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu, 2023.
Amesema wameridhika kuwa utekelezaji huo umefanyika kwa zaidi ya asilimia 80, na kwamba miradi imetekelezwa kwa ubora, na kusifu mipango bora iliyowekwa ya umaliziaji wa miradi inayoendelea.
"Mazuri ni mengi, matarajio ya kufika mbele ni makubwa" Amesisitiza Katibu Sankwa.
Katika siku ya pili ya ziara, Kamati imetembelea mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kisimatui, Kituo cha Afya Pongwe, Jengo la Kitega Uchumi linalojengwa kituo cha mabasi Kange, na Mradi wa ufyatuaji wa matofali uliopo eneo la viwanda, Gofu.
Katika mradi wa Zahanati Kisimatui, Mtendaji wa Kata ya Pongwe, Erica Njana, ameieleza Kamati kuwa mradi huo uliingiziwa fedha kiasi cha shillingi million 237 kwa ujenzi wa majengo mbalimbali ya huduma, na shillingi million 50 kwa ujenzi wa nyumba ya mtumishi. Zahanati hiyo inatarajiwa kuanza kutoa huduma katikati ya mwezi Desemba 2023 na kuhudumia zaidi ya wakazi 7000 wa Mitaa ya Kisimatui na Mgwisha.
Katika Kituo cha Afya Pongwe, Kamati ya Siasa Mkoa ilijionea utekelezaji wa miradi mitatu yenye jumla ya shillingi million 205.3, ya ukarabati wa Kituo hicho, ujenzi wa jengo la X-Ray na ujenzi wa jengo la TB na Ukoma.
Kamati pia ilitembelea na kukagua mradi wa jengo la kitega uchumi Kituo cha mabasi Kange ambao umefikia asilimia 97 ya utekelezaji, na gharama hadi kukamilika kwake ikikadiliwa kuwa shillingi billion 8.7.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.