Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Dennis Londo, imefanya ziara ya siku moja katika Jiji la Tanga, kutembelea miradi minne, ikiwemo Dampo la kisasa, barabara ya Msambweni na Makorora, maegesho ya malori Kange pamoja na Jengo la kitega Uchumi (Mall) inayojengwa stend ya mabasi ya mikoani na nje ya nchi, iliyopo Kange.
Akiongea katika ziara hiyo, Mhe. Londo amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga Dola zaidi ya 410 ya mradi wa Tactic kwa ajili ya kuboresha miundombinu na vitega uchumi kwa miji 45 ya Tanzania ikiwemo Jiji la Tanga, lengo likiwa ni kukuza uchumi na kuongeza pato la mtu mmoja-mmoja, na nchi kwa ujumla.
Hivyo amewataka wananchi kushirikiana kuilinda miundombinu hiyo ili iendelee kuwahudumia na kuongeza tija katika maisha yao, na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativile, pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga, Mhe. Mwantumu Zodo wakatumia Fursa hiyo kuwashauri wananchi pamoja na viongozi wa Jiji la Tanga kutunza miundombinu ya barabara pamoja na miradi inayotekelezwa na kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na tija ya kuweza kuendesha Jiji na taifa kwa ujumla.
(Story: Glory Machale.)
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.