Na. Mussa Labani, Tanga
Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Tanga, chini ya Mwenyekiti wake, Mstahiki Meya wa Jiji, Mhe. Al-Hajj Abdulrahman Shiloow, leo, Ijumaa Mei 26, 2023, imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa baadhi ya miradi ya ajira za muda inayotekelezwa chini ya mpango wa kunusuru kaya za walengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, TASAF.
Katika ziara hiyo, Kamati imetembelea mradi wa ujenzi wa kivuko cha miguu kilichopo Mtaa wa Mwahako barabarani, Kata ya Masiwani, Ujenzi wa kisima kifupi cha maji, kilichopo Mtaa wa Mapinduzi, Kata ya Duga, mradi wa usafishaji mfereji wa maji ya mvua, uliopo Mtaa wa Swahili Kata ya Magaoni, na upandaji wa miti ya kupendezesha mji pembeni ya barabara ya Jamathcan kuanzia shule ya Msingi Usagara, Kata ya Usagara.
Akizungumzia manufaa ya mradi wa ujenzi wa kisima kifupi cha maji katika Mtaa wa Mapinduzi kilicho gharimu kiasi cha shilling 820,000, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Athumani Mohamed Mganga, ameiambia Kamati ya Fedha kuwa wameupokea kwa furaha mradi huo kwani kisima hicho kimewawezesha kuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji kwa muda wote, tofauti na maji ya bomba ambayo kuna wakati hayatoki.
Mganga ameomba kuangaliwa uwezekano wa kupatiwa pump ili kuondoa adha ya kutumbukia kwa vichota maji, na kwamba maji hayo ni tegemeo kwa wakazi wengi wa mtaani kwake kwa matumizi ya nyumbani, ikiwa ni pamoja na kufua, huku akisifu uzuri wa maji hayo.
"Ila kuna changamoto kubwa ya watoto, watoto wadogo. Tumekubaliana kwenye vikao, kuwa mtoto chini ya umri wa miaka 14 asiruhusiwe kuteka maji ili kuepusha kutumbukia kisimani." amesema Mwenyekiti Mganga.
Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Jiji la Tanga Bw. Juma Mkombozi, amesema miradi iliyotekelezwa ilikuwa ni miradi midogo ambayo haikuhusisha uwekaji wa pump kwenye visima vya maji, hata hivyo amesema kipindi cha pili cha utekelezaji kitaanza hivi karibuni na kushauri iwapo jamii husika haitakuwa na hitaji jingine, wanaweza kutumia fedha za kipindi hicho kwa kuweka pump katika kisima chao, baada ya kupata ushauri wa kitaalam.
Awali, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Abdulrahman Shiloow, aliwataka wakazi wa eneo hilo kutoa mrejesho wa ubunifu unaofanywa na Serikali ambao una lengo la kutatua changamoto za wananchi na kurahisisha maisha yao.
Shiloow amesema pamoja na nafasi zao za kuwawakilisha wananchi, lakini pia wanasimamia shughuli za Serikali, hivyo wananchi wanapotoa mrejesho wa utekelezaji wa shughuli za Serikali kunawawezesha kujua mafanikio ya ubunifu huo.
Utekelezaji wa mradi wa ajira za muda katika Mpango wa kunusuru kaya za walengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, utasaidia kuinua uchumi wa kaya kwa kushiriki katika kazi za jamii na kupata kipato cha ziada kwa matumizi ya kaya, na wakati huo wakiboresha miundombinu katika jamii huku wakipata ujuzi na stadi za maisha.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.