Na. Salma Ramadhani
Julai 15, 2024.
Kamati ya kudhibiti Ukimwi ya Halmashauri ya Jiji la Tanga chini ya Mwenyekiti wake, ambae ni Naibu Meya wa Jiji, Mhe. Rehema Mhina, imefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi na shughuli zinazotekelezwa na vikundi vya watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (Waviu) na Waraibu wanaopata nafuu kutoka matumizi ya dawa za kulevya, kujionea namna wanavyoendesha shughuli zao za kujiletea maendeleo kwa fedha za ruzuku walizopokea.
Vikundi vilivyotembelewa leo, ambavyo ni sehemu ya vikundi 11 vilivyopokea ruzuku, ni pamoja na Baraza la Umoja wa Watu Wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (KONGA) ambapo wameweza kununua pikipiki na guta kwa shilingi milioni 11, kikundi cha Waviu Mchaka kilichopo katika Kata ya Duga kinachojishughulisha na shughuli za uuzaji wa vinywaji baridi na ushonaji wa nguo, ambacho kimepata shilingi milioni 2, kikundi cha Apple cha ushonaji na uuzaji wa vinywaji baridi, kimepata shilingi milioni 2, na kukagua kikundi cha waraibu wa dawa za kulevya wanaopata nafuu, cha ufugaji wa kuku kilichopo Makorora, nacho kikiwa kimepata ruzuku ya shilingi milioni 2.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Rehema Mhinda amesema kupitia agizo la Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kusisitiza tiba kazi, Halmashauri ya Jiji la Tanga imetoa shilingi milioni 30 fedha za ruzuku kwa ajili ya kuwawezesha watu waishio na maambukizi ya virusi vya ukimwi kufanya kazi za kujiingizia kipato.
Aidha ameshauri wananchi ambao wapo kwenye uraibu na ambao wameanza kunywa dawa pamoja na wanaoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi kujiunga kwenye vikundi pamoja na KONGA, ili kupewa elimu ya jinsi ya kuishi na kutumia dawa kwa usahihi na kupatiwa mikopo ya Halmashauri itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Mratibu wa Ukimwi Jiji la Tanga Bw. Moses Kisibo amesema kamati imeshauri kuwapatia elimu maafisa maendeleo ya jamii na maafisa kilimo na mifugo kutoka kwenye maeneo husika ili kuleta chachu mpya ya mabadiliko katika vikundi hivyo .
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.