Mussa Labani.
Dodoma, February 9, 2023.
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga wameanza ziara yao ya mafunzo katika Jiji la Dodoma kwa kutembelea miradi minne ya kiuchumi inayotekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani, ambayo inatarajiwa kuwa vyanzo vya uhakika vya mapato kwa Halmashauri hiyo.
Mara baada ya kufika katika Ofisi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma, msafara huo wa madiwani wa Jiji la Tanga unaoongozwa na Mstahiki Meya Mhe. Al-Hajj Abdulrahman Shiloow, ulipokelewa na Naibu Meya wa Jiji la Dodoma, Mhe. Jamal Ngalya na Mkurugenzi wa Jiji hilo Bw. Joseph Mafuru, ambapo waliweza kupata taarifa za utekelezaji wa miradi na matarajio ya Halmashauri hiyo kwa miradi hiyo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mkurugenzi wa Jiji Bw. Joseph Mafuru amesema Halmashauri hiyo inatekeleza miradi mingi mikubwa kwa fedha za ndani kwa kujinyima, na kuwekeza katika ujenzi wa miradi ya kiuchumi ili katika siku za usoni, Halmashauri isitegemee kuendesha shughuli zake kwa ushuru wa kukimbizana na wachuuzi wadogo, bali iwe na uhakika wa kupata mapato kutoka katika vitega uchumi vyake.
Mafuru amesema Halmashauri hiyo inajenga jengo la kitega uchumi katika eneo la Mtumba (Mtumba Complex) kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza wanajenga jengo la hotel ya ghorofa 5 na kumbi za mikutano 7, kati ya hizo ukumbi mmoja mkubwa ukiwa na uwezo wa kuchukua watu 1000 kwa wakati mmoja, kwa gharama za mradi zikiwa ni shillingi Billion 59.3.
Halmashauri hiyo pia imetekeleza mradi wa ujenzi wa soko la wazi la Machinga (Machinga Complex) mradi uliogharimu zaidi ya shillingi Billion 9.5, ambapo fedha za mapato ya ndani zikiwa ni shillingi Billion 6.5 huku zaidi ya Machinga 3,000 wakiingia na kufanya biashara zao kwa uhuru.
"Kuna faida nyingi zimepatikaa kwa ujenzi wa lile soko. Kwanza kwa sasa hata mvua zinyeshe, jua haviwapati. Wapo kivulini. Jiji sasa ni safi, sasa hivi unaweza kuiona barabara hadi mwisho, palikuwa pachafu.
Pale kwa sasa hawalipi, lakini tumewapa muda, muda ukiisha wataingia mikataba ambayo watalipa na tunatarajia kukusanya shillingi Billion 1.5 kwa mwaka.
Lakini pia kuna fursa zingine zimejitokeza. Kama kuna maombi ya kuweka mbao kubwa za matangazo(Billboards), kwenda kufanya matamasha, vibanda vya ATM, ambao pia wanalipia" amesema Bwana Mafuru.
Katika ziara hii, madiwani wameweza kutembelea jengo la kitega uchumi la Mtumba, stendi kuu ya mabasi - nanenane, mradi wa Machinga Complex na mradi wa Hotel ya Dodoma Jiji(Dodoma City Hotel) ambapo katika miradi yote hiyo, wamepongeza Jiji la Dodoma kwa uwekezaji mkubwa walioufanya.
Katika stendi kuu ya mabasi, Meneja wa stendi hiyo Bw. Mabrouk Seif alisema stend hiyo hupokea wastani wa mabasi 300 hadi 350 kwa siku na zipo huduma mbalimbali ambazo hutolewa na kituo hicho ikiwemo kumbi, kulaza mabasi na magari binafsi.
Waheshimiwa Madiwani waliweza kujionea mradi wa hotel ya Dodoma City Hotel yenye vyumba vya kulala 85, ambapo mradi huo umegharimu kiasi cha shillingi Billion 11.9 na tayari imepata mwendeshaji.
Jioni ya siku ilikamilika kwa Waheshimiwa Madiwani kukutana na Mbunge wa Jiji la Tanga na ambaye pia ni Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu kwa kikao cha kusalimiana na kubadilishana mawazo.
Na siku ya ijumaa asubuhi Waheshimiwa Madiwani watahudhuria kikao cha Bunge.
Wilaya ya Dodoma ilianzishwa mwaka 1973, mwaka 1980 ilipewa hadhi ya kuwa Manispaa na tarehe 26 April 2018 ilipewa hadhi ya kuwa Jiji.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.