Mussa Labani, Tanga.
Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Tanga wa robo ya pili kwa Mwaka wa fedha 2022/2023 uliofanyika Jumatano, Februari 01, 2023, umepokea na kuridhia taarifa ya Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Al-Hajj Abdulrahman Shiloow juu ya uamuzi wa Halmashauri kujitoa katika Sakata la uhalali wa umiliki wa eneo la Uwanja wa Mzalendo, uliopo Kata ya Mwanzange karibu na Soko la Mgandini.
Akisoma taarifa ya Mstahiki Meya kwa Baraza, Al-Hajj Shiloow amesema Baraza la Madiwani halina maslahi yoyote na uwanja wa Mzalendo ambao katika mipango kabambe ya Halmashauri ya tangu mwaka 1963 ulidhamiriwa na kupangwa kuwa eneo la makaburi.
Aidha amesema kuwa, Mamlaka ya ubadilishaji wa michoro, matumizi ya ardhi kwa sasa Baraza pamoja na kamati zake halihusiki na halina mamlaka hayo.
Eneo hilo la uwanja wa Mzalendo kwasasa lipo chini ya Taasisi moja ya kidini kufuatia taratibu za kisheria kuonyesha wanahaki ya kumiliki.
Akizungumzia taswira ya Jiji, Mhe. Shiloow ametoa miezi mitatu (03) kwa wamiliki wa majengo mabovu, machafu au yaliyochoka yaliyo katikati ya Jiji kuyafanyia uwekezaji, kuyauza au kuyarekebisha ili yaendane na hadhi ya Jiji la Tanga.
Mstahiki Shiloow ametumia pia mkutano huo kuwataka wasafirishaji wote kuanza na kumalizia safari zao kwa kupita katika stendi ya Jiji iliyopo Kange, na kwa wale wenye terminal (vituo vyao) ambao wamekidhi vigezo, wakitakiwa kupita Kange Stendi dakika 15 kabla ya muda wa kuanza safari na wakilazimika kupita wakirudi safari.
Mkutano huo wa kawaida wa Baraza la Madiwani ulianza kwa kuapishwa kwa Diwani mpya wa Kata ya Mnyanjani Mhe. Simba M. Kayaga wa Chama Cha Mapinduzi ambaye alichaguliwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni kujaza nafasi ya Marehemu Yakub Nuru Othman aliyefariki Mei 15, 2022.
Awali, Meya Shiloow alimpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt. Sipora J. Liana kwa kuiongoza Menejimenti ya Halmashauri katika ukusanyaji wa mapato, na hivyo Halmashauri kufanikiwa kuvuka lengo la makusanyo ya mapato kwa nusu mwaka (Julai – Desemba) kwa kuweza kufikia asilimia 50.4, na hivyo kuongoza kimkoa kwa makusanyo.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.