Halmashauri ya Jiji la Tanga linatarajia kutumia kiasi cha Bil 71.4 kwa shughuli zake kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/2019. Hayo yamesemwa leo, Ijumaa na Mkurugenzi wa Jiji hilo Bw. Daudi Mayeji kwenye kikao maalum cha Baraza la Waheshimiwa Madiwani akiwa anawasilisha mapendekezo ya Mpango wa Bajeti wa Halmashauri hiyo kwa mwaka 2018/2019 kwenye ukumbi mkubwa wa mikutano wa Jiji hilo.
Akiwasilisha mpango huo mbele ya Waheshimiwa Madiwani wa Jiji hilo, Mkurugenzi Mayeji alisema, mpango huu umezingatia miongozo yote iliyotolewa na Serikali.
Halmashauri ya Jiji la Tanga katika Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/2019 inakadiria kutumia jumla ya Tshs. 71,425,275,223.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, ulipaji wa Mishahara na utekelezaji wa Miradi ya maendeleo. Halmashauri hii katika Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/2019 inakadiria kukusanya fedha kutoka Vyanzo vya Ndani, Ruzuku na Wahisani pamoja na Nguvu za Wananchi. Kutoka Vyanzo vya Ndani inakadiriwa kukusanywa kiasi cha Tsh. 15,192,895,182.00 kwa ajili ya matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo. Kwa upande wa Ruzuku kutoka Serikali Kuu na Wahisani inakadiriwa kupatikana kiasi cha Tshs. 55,732,380,041.00 kwa ajili ya Mishahara, Matumizi Mengineyo na Miradi ya maendeleo.
Akichangia kwenye Mpango huo, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Mustapha Seleboss alisema, anaishukuru Serikali kwa kuweka miongozo ambayo imekuwa ikitoa njia nzuri ya mipango yetu. “Mpango huu umegusa kila idara, tumegusa idara ya Mahakama tumeitengea Mil. 50, tumegusa Polisi na tumewatengea Mil. 50, hizi zote ni huduma za kijamii, lakini tumegusa maabara na vyoo vya shule ya sekondari na msingi, madarasa ya shule za msingi tumetenga zaidi ya Mil. 300” alisisitiza Mstahiki Meya. Akiendelea kuusemea mpango huo, Mstahiki Meya alizungumzia pia Halmashauri kutenga zaidi ya Mil 106 za kufungua barabara za pembezoni mwa Jiji.
Mbali na kuuzungumzia Mpango wa Bajeti, Mstahiki Meya alinena na Mhe. Mbunge Mussa Mbarouk na Mhe. Mbunge Nour Bafadhili ambao walikuwepo kwenye kikao hicho. “Waheshimiwa Wabunge, nyie mpo kwa ajili ya watu wa Tanga, ni lazima muangalie maslahi ya watu wa Tanga kwanza na si mambo mengine” amelikazia kwa viongozi hao kuachana na ushabiki wa vyama bali waangalie maslahi ya watu wa Tanga.
Alisema hayo kufuatia kwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kususia na kutoka Bungeni wakati masuala ya msingi yakiendelea kujadiliwa, hivyo kuwaomba Wabunge hao kutotoka kwenye Vikao kwani kufanya hivyo ni kuwapotezea nafasi watu wa Tanga.
Nae Mbunge ya Jimbo la Tanga, Mhe. Mussa Mbarouk akichangia kwenye kikao hicho, alisema ya kwamba pamoja na Mpango huu kuonekana kuwa ni mzuri ni lazima kuwe na usimamazi mzuri wa makusanyo ili yale yote yaliyo kwenye Mpango yafanyike kama yalivyopangwa, na wao wataendelea kuyasemea pia kwenye ngazi ya Bunge kuanzia kwenye Kamati hadi kwenye Kikao cha Bajeti.
Mhe. Mussa pia alitoa shukrani kwa Serikali kwa kuleta fedha za afya kwa kutanua huduma ya afya kwa upande wa akina mama kwenye masuala mazima ya uzazi na kusisitiza kwa Waheshimiwa Madiwani kuwe na ufuatiliaji na usimamizi mzuri. “Serikali imetuletea bil. 1.4 kwa vituo vyetu vya afya vya Makorola, Mikanjuni na Ngamiani, Madiwani wa kata hizo wasiwe mbali na miradi hiyo”
Baada ya majadiliano, Mpango huo ulipitishwa na Kikao hicho hivyo kuwa Mpango rasmi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga na kisha kwenda kuwasilishwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa hatua za mbele zaidi.
Utekelezaji wa Bajeti ni suala la Kisheria na unazingatia majukumu ya Halmashauri kama yanavyoainishwa katika Sheria ya Serikali za Mitaa Na 9 ya mwaka 1982. Utekelezaji huu utaendana na Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 na Kanuni za Bajeti za mwaka 2015, usimamizi wa Sheria ya fedha ya Serikali (Public Finance Act Cap.348), Sheria ya manunuzi ya Serikali ya mwaka 2011 (Public Procurement Act Cap.410), Sheria ya Tawala za Mikoa, Sheria ya fedha ya serikali za Mitaa ya mwaka 1982 na marekebisho ya mwaka 2000 (Local Government Finance Act Cap.290), Sheria ya Utumishi wa Umma No.8 ya mwaka 2002 na marekebisho ya Sheria Na.8 ya mwaka 2007 na Miongozo na nyaraka mbalimbali za serikali.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.