Na; Mussa Labani
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Jiji la Tanga limepokea taarifa ya rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa mwaka 2023/2024 iliyowasilishwa leo, alhamisi Machi 2, 2023 katika mkutano maalum wa Bajeti ulioanza leo na kutarajiwa kuisha hapo kesho.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Afisa Bajeti kutoka Idara ya Mipango, Mchumi Maria Ndohelo amesema maandalizi ya Bajeti hiyo yamefuata utaratibu wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali (Budget Cycle), sera na miongozo ya Kitaifa na ya Kisekta pamoja na mipango na mikakati mbalimbali, ikiwemo ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya Mwaka 2020 - 2025.
Mkutano huo wa Baraza ulioongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Al-Hajj Abdulrahman Shiloow, na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tanga Meja (Mst) Hamisi Mkoba, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Hashim Mgandilwa, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt. Sipora Liana, ulipitia taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka 2021/2022, na nusu mwaka ya utekelezaji kwa mwaka 2022/2023.
Katika taarifa za mapitio, wajumbe walieleza kuridhishwa kwao na utekelezaji wa shughuli za Halmashauri, hasa katika eneo la ukusanyaji wa mapato ambapo katika mwaka 2021/2022, Halmashauri iliweza kuvuka lengo la makusanyo kwa kukusanya kwa asilimia 113 ya lengo la makusanyo ya mapato ya ndani, na katika kipindi cha nusu mwaka 2022/2023 kilichoanzia Julai hadi Desemba 2022, Halmashauri pia imeweza kuvuka lengo la makusanyo kwa kukusanya kwa asilimia 50.04.
Katika kipindi hicho pia, Halmashauri imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kutoka katika fedha za ndani, fedha za Serikali kuu, wafadhili na vyanzo vingine, ikiwemo miradi ya ujenzi wa vituo vya huduma ya afya, madarasa, matundu ya vyoo katika shule, jengo la kitega uchumi, utoaji wa mikopo, n.k.
Akitoa nasaha zake katika Baraza hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe Hashim Mgandilwa, ameshauri Halmashauri kufikiria kuanza miradi mikubwa ya uwekezaji itakayokuwa chanzo cha uhakika cha fedha, akitolea mfano wa ujenzi wa Hotel na kumbi za mikutano, ambazo zinaweza kuwekezwa hata nje ya mipaka ya Jiji au nje ya Mkoa wa Tanga.
Mgandilwa pia ameshauri Jiji kuweka utaratibu wa kuandaa maandiko ya kitaalamu kwa ajili ya kuomba fedha za kuanzisha miradi ya uwekezaji badala ya kusubiri za kuletewa.
Katika siku yake ya pili ya mkutano, Baraza litapokea na kujadili mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2023/2024 ambapo makisio ya kukusanya na kutumia jumla ya shillingi 72,111,627,000.00 (Billion 72.1) kwa ajili ya mishahara na matumizi mengineyo, yatawasilishwa.
Mkutano huu ni muendelezo wa vikao vya maandalizi ya Bajeti ya Halmashauri ambapo tayari umetanguliwa na vikao vya Menejimenti, wadau, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC), Baraza la Wafanyakazi, na Kamati za Kudumu za Halmashauri, ambapo kesho ijumaa Machi 3, 2023 vinahitimishwa katika siku ya pili ya Mkutano wa Baraza la Madiwani tayari kwenda ngazi ya Mkoa, Wizara na hatimaye Bungeni.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.