Na; Mussa Labani, Tanga.
Wito umetolewa kwa Wazazi na Walezi katika Jiji la Tanga, wenye watoto waliofikia umri wa kuanza shule katika madarasa ya awali na darasa la kwanza, kuwaandikisha kabla au ifikapo Desemba 30, 2022, tarehe iliyopangwa kama muda wa ukomo wa uandikishaji watoto kwa mwaka wa masomo unaoanza Januari 2023.
Wito huo umetolewa alhamisi, Desemba 22, 2022, na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Al-Hajj Abdulrahman Shiloow wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya hali ya uandikishaji wa wanafunzi kwa madarasa hayo.
Al-Hajj Shiloow amesema, tofauti na ilivyozoeleka kwa miaka mingi iliyopita kuwa, uandikishaji huendelea kwa miezi hadi mitatu tangu shule kufunguli, lakini kwa wakati huu, Serikali imepanga zoezi hilo kufungwa mwisho wa mwezi huu wa Desemba, hii ni kuwezesha watoto wote kuanza masomo kwa pamoja kuondoa muachano wa ufundishaji.
"Naomba nichukue fursa hii, kuwaomba na kuwasihi, wazazi na walezi katika Jiji hili la Tanga, na maeneo mengine yote ya Tanga, kwamba uandikishaji wa watoto katika madarasa yetu ya awali na la kwanza, utamalizika tarehe 30 Desemba.
Niwaombe shime wazazi wote, wenye watoto wa kike na kiume, wenye ulemavu na wasio na ulemavu, mwisho ni tarehe 30 mwezi huu, shule zipo wazi, walimu wapo kwa ajili ya shughuli za shule, uandikishaji unaendelea katika shule zote 81 za Halmashauri, uandikishaji ni bure, hakuna kitu chochote utakacho chajiwa." Amesisitiza Mstahiki Meya Shiloow.
Umri wa kuandikishwa kwa wanafunzi wa darasa la awali ni miaka 4, wakati wale wa darasa la kwanza ni miaka 6.
Kwa mujibu wa takwimu zilivyo sasa, wanafunzi walioandikishwa kwa darasa la awali katika shule za Serikali kwa Jiji la Tanga ni 3,122 kati ya matarajio ya kuandikisha watoto 6,417 hii ni sawa na asilimia 48.6 ya lengo.
Na kwa darasa la kwanza walioandikishwa ni 5,882 kati ya matarajio ya kuandikisha watoto 9,397 ikiwa ni sawa na asilimia 62.5 ya maoteo ya uandikishaji.
Aidha, Shiloow amewasihi wazazi na walezi kutoa kipaumbele katika lishe kwa watoto wanapokuwa shuleni kwa kuchangia gharama za utoaji chakula jambo litakalosaidia kuongeza uelewa darasani kwani lishe hujenga afya ya akili na mwili kwa mtoto.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.