Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Rehema Mhina, amelipongeza Shirika lisilo la Serikali, linaloshughulikia usalama barabarani la Amend, kwa kutekeleza mradi wa usalama barabarani maeneo ya shule, uliosaidia kupunguza ajali, hasa kwa watoto na kuwaimarishia usalama wanapotumia barabara.
Mheshimiwa Mhina ametoa pongezi hizo wakati wa hotuba yake ya kufunga rasmi mradi wa usalama wa watoto barabarani uliotekelezwa na shirika la Amend chini ya ufadhili wa Fondation Botnar, katika maeneo ya shule za msingi na sekondari zipatazo kumi na tano (15) kwa kipindi cha miaka minne (2019 - 2023), ikihusisha ujenzi wa vivuko vya waenda kwa miguu, utoaji wa elimu ya matumizi salama ya barabara kwa watoto mashuleni, mafunzo kwa bodaboda na uhamasishaji wa watu kufuata sheria za barabara.
"Jukumu la kuhakikisha usalama wa watoto wetu ni letu sote. Wafadhili wa mradi huu, Botnar na watekelezaji wa mradi, Shirika la Amend, wamefanya mambo ya muhimu katika kutuboreshea miundombinu yetu katika kuhakikisha usalama wa watoto wetu, na natoa rai kwa watu wote kuendelea kuhamasisha matumizi salama ya barabara" amesisitiza Naibu Meya Mhina.
Naibu Rehema Mhina ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafadhili kuleta miradi ya kuwanufaisha wananchi, na kwa nia ya dhati ya kuhakikisha usalama wa watoto pale wanapotumia barabara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania, Ndg. Simon Kalolo, amesema barabara salama ni haki ya msingi kwa binadamu wote, lakini watoto wanafaa kupewa upekee zaidi katika safari yao ya kwenda shuleni, na kwamba hawapaswi kuwekwa kwenye hatari ya ajali za barabarani.
Mkutano huo wa kufunga rasmi mradi wa usalama wa watoto barabarani, ulifunguliwa kwa njia ya video na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Alhaj Abdulrahman Shiloow, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Madiwani, Mwakilishi wa Fondation Botnar, Viongozi kutoka Polisi kikosi cha Usalama barabarani, Walimu na wanafunzi, viongozi wa bodaboda, na wengineo katika usalama barabarani.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.