Utangulizi
Tanzania bara (Tanganyika) imekuwa chini ya ukoloni wa wajerumani kuanzia mwaka 1884 hadi 1916 na Waingereza kuanzia mwaka 1917 hadi 1961. Tanganyika ilipata uhuru kwa njia ya amani.
Wilaya ya Tanga ni miongoni mwa Wilaya zilizoanzishwa wakati wa ukoloni ikiwa chini ya Jimbo la Kaskazini Mashariki ambalo Makao Makuu yake yalikuwa Tanga. Baada ya Uhuru mwaka 1961 Serikali iliendeleza mfumo wa kiutawala ngazi ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa baadae yalifanyika mabadiliko yaliyolenga kukidhi matakwa ya Serikali ya kizalendo. Awali Wilaya ya Tanga ilijumuisha Wilaya za Muheza , Mkinga na Tanga yenyewe
Kuanzia mwaka 1961 Wilaya ya Tanga imekuwa na Halmashauri ya Mji ambayo ilipandishwa hadhi kuwa Manispaa mwaka 1983 na kuwa Halmashauri ya Jiji mwaka 2005.
Jiografia na Mipaka
Jiji la Tanga lipo katika longitudo 38o53’ na 39o10’upande wa mashariki na latitudo 5o na 5o16’ Kusini mwa Ikweta. Jiji la Tanga lipo upande wa Kaskazini Mashariki mwa Tanzania, linapakana na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza upande wa Magharibi na Kusini, Kaskazini Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga na Mashariki bahari ya Hindi. Tanga iko umbali wa km 350 kaskazini mwa mji wa Dar es salaam na iko umbali wa Km 250 Kusini mwa Mji wa Mombasa.
Utawala
Wilaya ya Tanga inaongozwa na Mkuu wa Wilaya akisaidiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanga kwa upande wa Serikali Kuu. Uongozi kwa upande wa Serikali za Mitaa unaongozwa na Mstahiki Meya na Mkurugenzi wa Jiji, Watendaji na Baraza la Madiwani.
Halmashauri ya Jiji la Tanga ina Mhe. Mstahiki Meya 1, ina jumla ya Madiwani 37 kati yao 27 ni wa kuchaguliwa na 10 ni Vitimaalum
Jiji la Tanga ndio Makao Makuu ya Mkoa wa Tanga. Jiji la Tanga lina jumla ya Tarafa 4, kata 27 na mitaa 181. Jiji la Tanga limegawanyika katika maeneo ya mjini na nje ya mji ambapo jumla ya kata 16 ziko mjini, na kata 11 nje ya mji. Jiji lina jimbo moja la uchaguzi ambalo ni jimbo la Tanga
Mgawanyiko wa Kata katika Jiji la Tanga
Tarafa
|
Kata za Mjini |
Kata za nje ya mji |
Jumla |
Chumbageni
|
2 |
4 |
6 |
Ngamiani Kati
|
7 |
- |
7 |
Ngamiani Kaskazini
|
6 |
- |
6 |
Pongwe
|
1 |
7 |
8 |
Jumla
|
16 |
11 |
27
|
Eneo la Jiji na tabia ya nchi
Jiji lina eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 600 hii inajumuisha sehemu ya eneo la bahari lenye ukubwa wa kilomita za mraba zipatazo 62. Tanga inaambaa kilometa 20 kutoka ukanda wa pwani katika mita za mwinuko kati ya 0-17 kutoka usawa wa bahari. Muonekeno wa Tanga ni milima midogo, mabonde na Mito.
Hali ya Hewa
Hali ya hewa ya Jiji la Tanga ni kama ile ya maeneo ya Pwani ambayo huwa na joto. Hali ya hewa ya Tanga ni nyuzi joto kati ya 24 – 33c. Jiji lina misimu miwili mikubwa ya mvua na mmoja mdogo. Misimu hiyo ni, Mvua za masika ambazo hunyesha kuanzia mwezi Machi hadi Mei, wakati ambapo Tanga hupata mvua za millimita 1000 hadi 1400. Mvua za vuli ambazo hunyesha toka mwezi Septemba hadi Desemba na kuleta mvua za milimita 500 hadi 800. Mvua za mchoo ambazo hunyesha toka Julai hadi Agosti na kuleta mvua ya milimita 100 kwa wastani.
Idadi ya watu
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Jiji la Tanga lina jumla ya watu 273,332 kati yao Wanaume ni 130,920 na Wanawake ni 142,412. Watu wanaoishi maeneo ya Mjini ni 221,127 sawa na asilimia 80.9 kati yao wanawake ni 116,708 na wanaume 104,419, wakati watu wanaoishi nje ya mji ni 52,205 sawa na asilimia 19.1 kati yao wanawake ni 25,704 na wanaume ni 26,501. Hii ni sawa na ongezeko la watu asilimia 4.2 (population growth rate) kwa mwaka. Kwa sasa idadi ya watu inakadiriwa kuwa ni 305,585.
Shughuli za Uchumi
Uchumi wa Jiji la Tanga unategemea shughuli za Viwanda, Biashara ndogo ndogo,kubwa na za kati, Uvuvi, Kilimo na Ufugaji.
Inakadiriwa kuwa pato la mwaka la mkazi wa Jiji la Tanga (2017) ni shilingi 1,772,613.00 Kiwango hiki kiko juu kidogo ukilinginisha na kiwango cha Mkoa ambacho ni wastani wa Tshs1,022,016.00 na kiko juu ya malengo tuliyojiwekea kimkoa ya kufikia 1,500,000 kwa mwaka kufikia mwaka 2020.
Juhudi zinazoendelea ni kutangaza na kutumia fursa zilizopo ndani ya Jiji la Tanga kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo na sekta za biashara, viwanda, masoko na miundombinu, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kuendelea na juhudi za kuondoa vikwazo ndani ya jamii na kupunguza urasimu katika kusaidia ukuaji wa kiuchumi kwa watu binafsi na kwa makundi maalumu katika jamii.
Bonyeza hapa kupata Orodha ya Wenyeviti na Mameya waliongoza Halmashauri kuanzia 1961 hadi sasa
Bonyeza hapa kupata Orodha ya Wakurugenzi waliongoza Halmashauri kuanzia 1961 hadi sasa...
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.