MHE UMMY ATOA WIKI TATU KITUO CHA AFYA TONGONI KUANZA KUTOA HUDUMA.
“Ahadi za miradi ya Afya na Elimu aanza kuzitekeleza”.
Na.Mwajuma Ernest.
Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mhe Ummy Mwalimu amefanya ziara katika Kata ya Tongoni na Kirare ikiwa ni moja ya utekelezaji wa majukumu yake.
Mhe Ummy akiwa katika Kata ya Tongoni ametembelea ujenzi wa Kituo cha Afya Tongoni ambacho ujenzi wa jengo la Wagonjwa wa nje(OPD)na jengo la maabara vimekamilika na ujenzi wa wodi ya wanawake na watoto umeanza ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 500 kimetolewa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mbunge. Mhe Ummy amemwagiza Mganga Mkuu wa Jiji kuhakikisha kituo hiki kinaanza kutoa huduma ifikapo tarehe 1/08/2022.
“Hapa naagiza kama Waziri ifikapo Agosti Mosi kituo hiki cha afya kianze kutoa huduma kwani majengo yamekamilika pamoja na miundombinu ya Maji Mganga Mkuu wa Jiji nadhani umenielewa”
Wakati huohuo Mhe Ummy ametembelea ujenzi wa nyumba ya Mwalimu katika Shule ya Sekondari Tongoni ambapo ameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa nyumba hiyo ambayo ina uwezo wa kukaa familia mbili za walimu. Mwaka 2021, Mhe Ummy alitoa ahadi ya kutafuta shilingi milioni 50 ili kujenga nyumba hiyo kwa lengo la kuboresha mazingira ya walimu baada ya kutembelea shule hiyo.
“Ahadi yangu ya ujenzi wa nyumba za waalimu naitekeleza nimeridhishwa na kasi ya ujenzi wa nyumba hii kwakweli hili litasaidia katika kuboresha elimu kwa kuwaweka waalimu karibu na shule”
Mhe Ummy pia aliendelea kusisitiza kuwa anaendelea kutafuta fedha ili shule hiyo iwe na kidato cha 5 na 6.
Aidha Mhe Ummy alikutana na wananchi na kusikiliza kero zao katika mtaa wa Tongoni, ambazo ilikuwa ni mikopo kwa wenye ulemavu, ujenzi wa zahanati Maere na ukosefu wa umeme Kiwavu. Kero nyingine ni maeneo mengi kuachwa mapori na wawekezaji na hivyo wananchi kukosa maeneo ya ujenzi.
Kuhusu swala la mikopo Mhe Ummy alimwagiza Afisa maendeleo wa kata kuhakikisha anakutana na vikundi hivyo ili awape elimu na kuwahakikishia wananchi wa Tongoni kuwa fedha za mikopo isiyo na riba kutoka halmashauri zipo,pia amewahakikishia wananchi wa Maere kuwa anatafuta fedha za ujenzi wa zahanati ya Maere.
Katika kata ya Kirare, Mhe Ummy alikutana na wananchi na kusikiliza kero zao ambazo ni pamoja na ubovu wa barabara na ukosefu wa umeme na alitembelea eneo ambalo wananchi wa Shaurimoyo na Kilombero wanaomba kujengewa shule shikizi ili kuwapunguzia umbali watoto wadogo wa maeneo hao.
Katika ziara hiyo Mhe Ummy aliambatana na Diwani wa kata ya Tongoni Mhe Nassoro Salimu na diwani wa kata ya Kirare Mhe Adam Mwagilo na mganga mkuu wa jiji Dr. Charles Mkombe ambapo walimpongeza Mhe Ummy na Mhe.Rais Samia Suluhu kwa kuendelea kuleta miradi mbalimbali katika jiji la Tanga.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.