ZAIDI YA SHILLINGI BILLION MOJA KUJENGA MLANGO WA CHUMA
Na: Mussa Labani
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Jiji la Tanga
Soko maarufu la Mlango wa Chuma lililopo kata ya Majengo Jijini Tanga, linatarajiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa utakaoligeuza soko hilo kuwa la kisasa lenye mandhari ya kuvutia na kuwezesha upatikanaji wa huduma zote muhimu katika masoko.
Akitoa taarifa ya hatua za maandalizi ya ukarabati huo, kwa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya ya Baraza la Madiwani wa Jiji la Tanga, Mchumi wa Jiji la Tanga, Bwana Simeon Vedastus Mzee ameieleza Kamati hiyo kuwa, tayari kiasi cha shillingi million 100 zimekwisha tolewa kwa kazi hiyo, na shillingi million 150 zimetengwa ili kufanya jumla ya shillingi million 250 kama fedha za awali huku mradi mzima ukitarajiwa kugharimu kiasi cha zaidi ya shillingi Billion moja.
Kwasasa taratibu zinafanyika za kuwahamisha kwa muda wafanyabiashara wa soko hilo ili kupisha kazi ya ujenzi, ambapo eneo linaandaliwa katika uwanja wa Chama cha Mapinduzi, Masiwani.
Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Mohamed Mfundo, ambaye pia ni Diwani wa Kiomoni, imefanya ziara ya kutembelea miradi ikiwa ni maandalizi ya vikao vya kamati vya robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Ziara hiyo ilianzia katika eneo la ufukwe Raskazone maarufu kama Jet ambako kamati ilikwenda kuona mazingira ya eneo hilo la kupumzikia na kupata taarifa za uendelezaji wa eneo hilo ambapo kamati ilitaarifiwa kuwa, tayari michoro iko tayari na fedha kiasi cha shillingi million 20 zimetengwa kwa ujenzi wa kibanda cha huduma na vinywaji katika eneo hilo.
Kamati ilitembelea shule ya msingi Bombo iliyopo kata ya Central kujionea uchakavu wa jengo la awali la shule hiyo linalokisiwa kujengwa mwaka 1902 ambalo kwa sasa halitumiki kutokana na kuwa hatarishi. Jengo hilo la ghorofa moja lililojengwa tangu enzi ya wakoloni, linanyufa kubwa, na maeneo mengine yakiwa tayari yamekatika na kuanguka.
Kamati pia ilitembelea kituo cha afya Mwakidila, katika kata ya Tangasisi, na Geza, kata ya Marungu, kuona eneo lililotengwa kujengwa Zahanati, pamoja na eneo la ujenzi wa soko la Machinga, lililopo kati ya maegesho ya Malori na kituo cha mabasi Kange.
Katika kituo cha afya cha Mwakidila, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dkt Catherine Rocky ameiambia kamati kuwa kituo kiliingiziwa shillingi million 238 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo la wagonjwa wa ndani (IPD), jengo la Utawala na jengo la huduma ya Mama na Mtoto.
"Katika ajira mpya zilizotoka, kituo chetu kitapata watumishi saba (7), ambapo miongoni mwao kuna madaktari wawili, manesi wawili, ila bado tuna mahitaji wa watumishi, hawatoshi" amesema Dkt. Rocky.
Katika mtaa wa Geza, kamati ilijionea eneo la ekari 3.5 patakapojengwa zahanati ya Geza na tayari kiasi cha shillingi million 225 zimetolewa na Halmashauri kwa kazi hiyo.
Kamati pia ilitembelea eneo la Machinga, ambapo kiasi cha zaidi ya shillingi million 540 kitaanza kazi ya ujenzi wa eneo hilo.
Baada ya kukamilika kwa ziara ya kamati za Mipango Miji siku ya jumatatu, na kamati ya Uchumi siku ya jumanne, siku ya alhamisi itafanyika ziara ya kamati ya kudhibiti UKIMWI na kumalizia na kamati ya fedha siku ya Ijumaa, Julai 29, 2022.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.