Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amezitaka halmashauri zote nchini kuweka bei ya chini katika kuuza viwanja kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, Waziri Mwijage ameyasema hayo leo akifungua maonyesho ya sita ya biashara ya kimataifa Mwahako jijini Tanga.
“Kwa kumuuzia bei cha chini huyu mwekezaji, kutamfanya asitumie mtaji wake wote kwa kununua kiwanja tuu, bali kutamfanya apate kiwanja na mtaji wa kuanza kujenga kiwanda ambacho kitatengeneza ajira kwa wananchi wengine kwa haraka. Na uwepo wa viwanda kuna faida mbili, moja halmashauri kupata mapato na ajira kwa wananchi wetu” alisema waziri Mwijage
Akiwa kwenye ufunguzi wa maonyesho hayo, Mwijage amesema kuwa jiji la Tanga ni sehemu inayoongoza kwa viwanda vingi hivyo wawekezaji waendelee kujitokeza ili kuendelea kukuza pato la taifa kiuchumi.
Pia amewapongeza wajasiriamali kwa kuendelea kukuza uchumi wa viwanda vidogovidogo na kuwataka vijana kufanya kazi kwa bidii kwani wao ndio mhimili mkubwa katika kuongezea kipato taifa .
Jiji la Tanga lipo kwenye mazingira mazuri ya kufanya uwekezaji hasa kwa kuzingatia eneo la uwepo wake. Jiji hili lina njia za usafirishaji kwa kutumia barabara, reli, ndege na usafiri wa majini kwa maana ya kuwepo kwa bandari. Miundombinu ya barabara zilizopo Jiji Tanga zinamfanya mwekezaji kufanya mawasiliano na mikoa yote nchini na nchi jirani ya Kenya kwa barabara za lami.
Maonesho ya kimataifa ya biashara yanafanyika Jijini Tanga kuanzia tarehe 26 Mei na kumalizika tarehe 6 Juni, yakiwa yanashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wajasiliamali, makampuni, mashirika na taasisi za serikali. Washiriki hao wanatumia maonesho hayo kuonesha shughuli wanazofanya, kuonesha bidhaa wanazozalisha, kuuza bidhaa, kutoa ushauri, kutatua kero hali kadhalika na kutoa huduma kwenye viwanja vya maonesho.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.