MSTAHIKI MEYA APOKEA MSAADA WA VIFAA TIBA
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Abdulrahman O. Shiloow amepokea msaada wa vifaa tiba kwa ajili ya maandalizi ya kambi ya Madaktari Bingwa wa magonjwa ya masikio, pua na koo (ENT) vyenye thamani ya zaidi ya shilling millioni 12.5, kutoka Shirika la United Help for Tanzanian Children (UHTC) na United Help for International Children (UHIC)
Hafla fupi ya makabidhiano hayo imefanyika katika Kituo cha Afya cha Mikanjuni, ambapo kwa upande wa UHTC na UHIC waliwakirishwa na Mkurugenzi wa UHTC Dkt. Regis J. Temba na Mwenyekiti Bw. Joseph Desideri Geheri.
Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Diwani wa Kata ya Mabawa Mhe. Athumani I. Babu, Mganga Mkuu wa Jiji Dkt. Charles Mkombe, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mikanjuni Dkt. Ummykulthum A. Kipanga, Wafanyakazi wa kituo cha afya Mikanjuni pamoja na wadau wengine.
Akisoma taarifa ya maandalizi ya kambi hiyo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mikanjuni Dkt. Ummykulthum A. Kipanga amesema Halmashauri imepanga kufanya kambi ya matibabu kwa kutumia madaktari bingwa wa magonjwa ya masikio, pua na koo (ENT) inayotarajiwa kuanza tarehe 10 hadi 15 mwezi Augosti 2022.
“Kambi hiyo inatarajiwa kuhudumia wagonjwa 300 (screening) ambao kati ya hao takribani wagonjwa 100 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji” amesema Dkt. Kipanga.
Na kwa upande wao, Mkurugenzi wa UHTC Dkt. Temba na Mwenyekiti Bw. Desideri wamesema shirika limekuwa likisaidia dawa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa Vituo vya Afya vya Mikanjuni, Pongwe na Mafuriko zenye thamani ya zaidi ya shilling million mbili kwa kila mwezi lengo likiwa ni kuwezesha watoto kuwa na afya iliyo bora na jamii inayowazunguuka wapate matibabu.
“Na kuhusu kambi kwa ajili ya matibabu ya ENT, UHTC imesaidia vifaa vyote vilivyoombwa kwa kuzingatia vifaa ni muhimu katika utendaji. Na mstahiki Meya tutakabidhi vifaa hivi pamoja na risiti tulizonunulia, na orodha ya vifaa vyote ipo, tutakabidhi” amesema Dkt. Temba.
Akipokea msaada huo, Mstahiki Meya Shiloow amemtaka Mganga Mkuu wa Jiji kuhakikisha vifaa vilivyotolewa vinatumika kama ilivyokusudiwa wakati wa kambi hapo mwezi Augosti.
“Uaminifu ni pamoja na kumfanya mfadhili atimize lengo lake la utoaji wa msaada. Sasa sio leo mkose gloves, muanze kuchomoa kwenye hizi, hapana. Mhifadhi vizuri ili kutimiza lengo la mtoaji wa msaada” amesisitiza Meya Shiloow.
Mheshimiwa Shiloow pia ametumia hafla hiyo kuwaasa watumishi wote wa kada ya afya katika Jiji la Tanga kuimarisha ‘customer care’ (huduma kwa wateja), akiwataka kutumia lugha nzuri akisema haoni sababu za watu kukimbilia huduma katika vituo vya afya vya binafsi wakati vituo vya Serikali (Halmashauri) vina staff (Wafanyakazi) wa kutosha.
Hivyo amewataka watumishi hao wa afya kuwahudumia wagonjwa kwa moyo mkunjufu na iwapo kuna mahali wanakwama, basi watoe taarifa.
Kambi ya mwaka huu inatarajiwa kuwa na madaktari bingwa kutoka Zanzibar.
Labani.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.