UWANJA WA NANE NANE MOROGORO KUGEUZWA DARASA.
Watoto kupata elimu bure.
Mussa Labani - Morogoro
Zikiwa zimebaki wiki mbili kuanza kwa maonyesho ya kilimo, mifugo na uvuvi, maarufu kama maonyesho ya nane nane, hapo Augosti 1, 2022, maandalizi kwa kanda ya mashariki inayojumuisha mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro yamepamba moto huku zikitarajiwa teknolojia mbalimbali za kisasa kufundishwa uwanjani hapo na kuufanya uwanja wa Mwalimu J. K. Nyerere uliopo Manispaa ya Morogoro kugeuka kuwa darasa la uboreshaji kilimo, mifugo na uvuvi.
Akizungumza wakati wa kikao cha pili cha Kamati Kuu ya mandalizi ya maonyesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Adam Malima ambaye ndiye aliyeongeza kikao hicho, amesema lengo kubwa la maonyesho hayo ni kuhakikisha kwamba wananchi wanaokuja kwenye maonyesho wanatoka na mbinu bora kwenda kuzalisha kwenye mashamba yao.
“Tunataka watu waje wajiulize. Kama linawezekana hapa, linawezekana shambani kwangu. Kwa hiyo akija atakutana na wenyeji wake (katika banda au vipando) atauliza maswali, tunataka kila kinachoonekana hapa kiweza kutafsirika na kupelekwa kwenye mashamba ya wakulima huko kwenye maeneo yao” amesema Malima.
Aidha Kamati Kuu imeamua kufuta kiingilio cha shilling Mia Tano (500) kinachotozwa kwa watoto, na hivyo kwa kuanzia maonyesho ya mwaka huu, watoto wataingia bure na kuweza kupata elimu kwa kuona kwa vitendo tofauti na shuleni ambako ni nadharia pekee.
Katika kuboresha teknolojia za kilimo, mifugo na uvuvi, Halmashauri zinazounda kanda ya Mashariki (kutoka Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro) na wadau wamehamasishwa na Kamati Kuu kuandaa vipando vinavyoweza kuchukua muda mfupi ili wananchi waweze kujifunza.
Wameshauriwa pia kutoa elimu ya namna bora ya uaandaji wa mashamba, upandaji, uvunaji na uhifadhi wa mazao. Kwa upande wa mifugo, Halmashauri na wadau wanashauriwa kuonesha teknolojia zinazohusiana na uongezaji wa tija katika uzalishaji kwenye mifugo, huku ukitolewa mfano wa uhimilishaji, uzalishaji na uhifadhi wa malisho kwa kutumia teknolojia rahisi kama vile mashine za kuchanganyia chakula.
Katika maonyesho hayo ambayo yamezidi kuvutia washiriki wa ndani ya nje, katika sekta ya uvuvi, Kamati Kuu imewataka waoneshaji kuonyesha mbinu rahisi za kuongeza tija katika uzalishaji wa samaki kama utengenezaji wa chakula bora, uzalishaji wa vifaranga bora vya samaki na uoneshaji wa zana sahihi zinazotumika katika uvuvi, kilimo cha mwani, unenepeshaji wa majongoo bahari na kaa.
Kikao cha Kamati Kuu ya maandalizi ya maonyesho ya kilimo, mifugo na uvuvi – Nane nane kwa Kanda ya Mashariki, kimefanyika katika ukumbi uliopo katika banda la maonyesho la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ndani ya uwanja wa maonyesho wa nane nane Manispaa ya Morogoro kikitanguliwa na Kikao cha Kamati ya Wataalamu kilichokaa siku moja kabla, na wajumbe wa Kamati Kuu wakiwa ni Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, pamoja na wataalamu wao kutoka Sekretarieti za Mikoa, Wakuu wa Sehemu za Mifugo na Kilimo pamoja na Maafisa Mawasiliano Serikalini kutoka mikoa inayounda kanda ya maonyesho.
Maonesho ya mwaka huu, yanafanyika baada ya kusitishwa mwaka 2021 na kisha kurejeshwa tena mwaka huu 2022. Kauli Mbiu ya Maonesho ya Nane Nane mwaka 2022 ni “Ajenda 10/30: Kilimo ni Biashara, Shiriki Kuhesabiwa kwa Mipango Bora wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi”
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.