Katika kuhakikisha sera ya elimu bure kutoka kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli inatekelezwa, Serikali inatoa zaidi ya milioni 200 kwa kila mwezi katika Jiji la Tanga ili kuboresha elimu. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kwenye uzinduzi wa majengo mapya ya shule ya msingi Bombo iliypo kata ya Central jijini Tanga.
Akizungumza katika ufunguzi huo Mhe. Ummy amesema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha inatatua changamoto za elimu nchini, ambapo kwa jiji la Tanga katika shule za msingi serikali imetenga milion 50 na sekondari imetenga milion 108.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Bw.Daudi Mayeji amebainisha mikakati iliyofanywa na halmashauri ili kuhakikisha shule hiyo inakuwa ya kisasa na wanafunzi waweze kujisomea katika mandhari nzuri. “Tulichukua maamuzi ya haraka, kwanza kabisa kusimamisha matumizi na kuwapeleka shule ya jirani, kisha kuanza kufanya ujenzi mpya kwa kiwango bora kama inavyoonekana” alisema Mkurugenzi Mayeji
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Madiwani katika shughuli ya kukabidhi majengo hayo kwa uongozi wa shule hiyo, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mustapha Selebosi ameeleza kuwa halmashauri imechangia zaidi ya milioni 279 kutoka kwenye mapato yake ya ndani. Meya pia, aliendelea kwa kuishukuru serikali kwa kupatia Jiji la Tanga fedha zaidi ya milioni 136 kupitia mradi wa Matokeo Kwanza “Education Programme For Results (EP4R)” ambazo nazo zimewasaidia sana kwenye kuimarisha na kuboresha miundombinu ya shule nyingine jijini humo.
Nao wanafunzi wa shule hiyo walionesha kufurahia kitendo cha kukabidhiwa shule yao. “Tunaishukuru halmashauri kwa kutujengea madarasa mapya, tumefurahi kwani ni madarasa mazuri na sasa tutasoma vizuri zaidi maana kule tulipopelekwa kwa muda tulikuwa tupo wengi darasani lakini sasa tutakaa vizuri na kusoma vizuri pia” walisema baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo.
Shule ya msingi Bombo ni miongoni mwa shule tatu za umma zilizopo ndani ya kata ya Central ikiwa na jumla ya wanafunzi 1158 wavulana wakiwa 620 na wasichana 538 huku jumla ya walimu 23 wanaume 3 na wanawake 20.
Shule hii ilijengwa mwaka 1902 na kuanza kutumika kama shule ya awali mwaka 1945 ikimilikiwa na Taibal Sachak kabla ya kutaifishwa na serikali baadae ilianza kutumika kama shule ya msingi hadi mnamo mwaka 2015 ilipositishwa matumizi kutokana na uchakavu hatarishi.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.