Shirika la Maendeleo ya Wanawake wa mkoa wa Tanga (Tanga Women Development Initiative - TAWODE) chini ya Mwenyekiti wake Mhe Ummy Mwalimu (Mb.) leo wameweka saini Mkataba wa Ujenzi wa Madarasa 6 ya Shule ya Msingi Mwakidila, iliyopo kata ya Tangasisi, katika jiji la Tanga. Msaada huo wenye thamani ya Dola za Kimarekani 84,000 (takriban shilingi za kitanzania milioni 188) umetolewa na Serikali ya Japan kupitia Ubalozi wa Japan nchini Tanzania kufuatia maombi ya Mwenyekiti wa TAWODE Mhe Ummy Mwalimu ya kuunga mkono Jitihada za Serikali za kuboresha Miundombinu ya Elimu ya Msingi na Sekondari katika Jiji la Tanga.
Akiongea wakati wa hafla hiyo
Mheshimiwa Masaharu Yoshida, Balozi wa Japan nchini Tanzania amesema, Serikali ya Japan inatoa fedha hizo ili kusaidia Maendeleo ya Elimu kwa Jiji la Tanga ili kutatua tatizo la mrundikano wa wanafunzi madarasani. Mheshimiwa Balozi Yoshida ameitaka TAWODE kuhakikisha Mradi huo unatekelezwa kikamilifu na kukamilika kwa wakati.
Mgeni Rasmi katika Uzinduzi huo Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto na Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Tanga ameushukuru Ubalozi wa Japan kwa kukubali ombi lao la kufadhili ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Mwakidila ambayo ina wanafunzi zaidi ya 1,400 kulinganisha na madarasa machache yaliyopo na hivyo kusababisha mrundikano mkubwa wa wanafunzi. Mhe Ummy alieleza kuwa Ongezeko la wanafunzi limechangiwa na uamuzi mzuri wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais, Dr. John Pombe Magufuli wa kutoa Elimu Bure. Na hivyo wakati Serikali ikiweka jitihada kubwa za kuboresha miundombinu ya Elimu katika Halmashauri mbalimbali kote nchini bado zipo changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa madarasa. Hivyo wao kama sehemu ya wanajamii wa Jiji la Tanga waliona wana wajibu wa kuunga mkono Serikali kwa kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuwezesha Elimu ya Msingi mpaka kidato cha nne kutolewa Bure bila vikwazo vyovyote.
Mhe Ummy alieleza kuwa Fedha zilizotolewa na Ubalozi wa Japani ni za Jamii ya wanaTanga, kwa Maendeleo ya Tanga. Hivyo Shirika la TAWODE kwa kushirikiana na Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji la Tanga itahakikisha msaada huu unatumika kikamilifu na mradi kukamilisha kwa wakati ili kupunguza changamoto ya mrundikano wa wanafunzi madarasani.
Kwa upande wake, Mhe Selebosi Mustafa Mhina, Meya wa Jiji la Tanga ameushukuru Ubalozi wa Japani kwa kufadhili ujenzi wa madarasa hayo. Na pia amemshukuru na kumpongeza Mhe Ummy Mwalimu kwa kuwa nao bega kwa bega katika kusukuma mbele maendeleo ya Wananchi wa Jiji la Tanga hasa katika Sekta ya Afya na Elimu. Mhe Meya pia amemkaribisha Balozi wa Japan kutembelea Tanga ikiwemo Shule ya Sekondari Japani iliyojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan.
Independent Avenue
Sanduku la Posta : P.O.BOX 178, Tanga
Simu ya Mezani: 027 2643068
Simu ya Mkononi:
Baruapepe: info@tangacc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Jiji la Tanga . Haki Zote Zimehifadhiwa.